Mbunge wa upinzani Tanzania Lissu apigwa risasi
7 Septemba 2017Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Mwigulu Nchemba anasema mwanasiasa huyo wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, alijeruhiwa na mshambuliaji asiyejulikana.
Nchemba anasema serikali itatoa taarifa baada ya kupata ripoti ya hali ya afya ya Lissu, ambaye pia ni rais wa chama cha mawakili, Tanganyika Law Society. Lissu ni miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaoikemea na kuikosoa serikali. Mwanasiasa huyo amefanyiwa upasuaji wa dharura baada ya kupigwa risasi tumboni na watu wasiojulika nje ya nyumbani kwake mjini Dodoma.
James Kiologwe, daktari katika hospitali kuu ya Dodoma amesema Lissu yuko katika hali imara.
Mwezi Julai mwaka huu alishtakiwa kwa kutumia lugha ya matusi baada ya kumuita rais John Pombe Magufuli dikteta kuhusina na madai ya kuushambulia na kuukandamiza upinzani na vyombo vya habari.
Taarifa kutoka chama cha upinzani CHADEMA imesema "mbunge huyo amejeruhiwa vibaya." Lissu alikuwa bungeni mapema leo na alikuwa akipelekwa nyumbani ndani ya gari lake wakati shambulizi hilo lilitokea.
Rais John Pombe Magufuli alisifiwa sana kwa kuanzisha vita vikali dhidi ya ufisadi tangu mwaka wa 2015 lakini anakosolewa kutokana na uongozi wake wa kimabavu dhidi ya upinzani na vyombo vya habari.
Matangazo ya moja kwa moja ya mijadala ya televisheni yalisimamishwa, na mikutano ya upinzani imepigwa marufuku hadi kipindi cha uchaguzi ujao wa 2020 kitakapofika.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu