Serikali ya Meloni yatimiza mwaka mmoja madarakani
25 Septemba 2023Waziri mkuu Meloni amekiri angeweza kufanya "vyema" katika kudhibiti wimbi la wahamiaji ambao wamezidi kuongezeka tangu chama chake cha mrengo wa kulia kiliposhinda uchaguzi wa kihistoria mwaka mmoja uliopita.
Katika mahojiano aliyoyafanya mwishoni mwa wiki na kituo cha utangazaji cha TG1, Meloni amesema hali iliyopo kwa hivi sasa sio matokeo waliyotarajia na kulitaja suala la uhamiaji kuwa tatizo gumu lakini anayo matumaini kwamba watalitafutia mwafaka.
Chama cha Meloni cha ndugu wa Italia, kilichaguliwa kwa kura nyingi baada ya kuahdii kulishughulikia wimbi la wahamiaji wanaoingia Italia. Lakini badala yake idadi ya wahamiaji wanaowasili kwa maboti kutokea Afrika Kaskazini imeongezeka, huku mwaka huu pekee wahamiaji wapatao 130,000 wakiwa wameorodheshwa na wizara ya mambo ya ndani kutoka idadi ya wahamiaji 70,000 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Mzozo huo ulishika makali baada ya wahamiaji 8,5000 kuwasili katika kisiwa kidogo cha Lampedusa ndani ya kipindi cha siku tatu mapema mwezi huu, hali iliyomlazimu Meloni kuutaka Umoja wa Ulaya kuchukua hatua za kuisaidia Italia ili kupunguza mzigo. Umoja wa Ulaya ulikubali kuzidisha juhudi ikiwa ni pamoja na kuanza kuipatia fedha Tunisia iweze kudhibiti wahamiaji wanaondoka nchini humo.
Lakini mshirika mkuu katika serikali ya Meloni, Matteo Salvini ambaye anatoka chama kinachopinga wakimbizi cha League party amekuwa akipuuzilia mbali juhudi za Umoja wa Ulaya kudhibiti ongezeko la wahamiaji wanaowasili aliowaita "kitendo cha vita".
Naibu huyo waziri mkuu ambaye alifunga bandari za Italia kwa mashirika ya kuwasadia na kuwaokoa wahamiaji wakati alipokuwa madarakani mwaka 2019, bado anashinikiza mwelekeo wa hatua kali zaidi.
Waziri Mkuu wa Italia aapa hatua kali kuzuia wahamiaji
Tangu kuingia madarakani mwaka mmoja uliopita, serikali ya Meloni imezuia shughuli za meli za kuwaokoa wahamiaji, ikizishutumu kwa kuwatia moyo wahamiaji na kuapa kushughulikia biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
"Wanatoza maelfu ya dola kwa safari za kwenda Ulaya, ambazo wanaziuza kwa vipeperushi kana kwamba ni mashirika ya kawaida ya usafiri. Lakini vipeperushi hivyo havisemi kwamba mara nyingi safari hizo husababisha kifo, kwenye kaburi lililo chini ya Bahari ya Mediterania,” alisema Meloni.
Serikali yake pia inataka kuongeza juhudi za kuwarejesha wahamiaji waliowasili lakini ambao hawajastahiki kupata hifadhi, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vipya vya vizuizi na kuongeza muda wa wahamiaji kuzuiliwa ndani ya vituo hivyo.
Pia ilifahamika wiki hii kwamba nchi hiyo itawataka wahamiaji watakaokuwa wanasubiri uamuzi wa maombi ya hifadhi kulipa kiasi cha euro 5,000 au kupelekwa kwenye vituo vya vizuizi, hatua ambazo zimekosolewa kwamba nchi hiyo inatoza "fedha za ulinzi".