1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Malawi Chakwera azuru Tanzania kuimarisha uhusiano

7 Oktoba 2020

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera yuko nchini Tanazania kwa ziara ya siku tatu kuimarisha uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania. Chakwera alipokelewa na mwenyeji wake rais John Magufuli jijini Dar es Salaam.

https://p.dw.com/p/3jZmq
Tansania Offizieller Besuch des Präsidenten von Malawi in Tansania
Picha: Department of information and communication of Tanzania

"Ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano kati ya mataifa mawili jirani, " alisema waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudikatika taarifa.

Akizungumza ikulu jijini Dar es salaam baada ya kumaliza mazungumzo yao ya faragha, Rais Chakware amesema kuna umuhimu mkubwa wa nchi za Afrika kuanza kujitamulisha upya kuhusu demokrasia wanayotaka.

Amesema hakuna haja tena kuendelea kukumbatia demokrasia inayotoka nje ya mipaka ya bara hili kwa kualika waangalizi wa kimataifa ambao mara zote ripoti zao haziakisi moja kwa moja matakwa ya kiafrika.

Rais Chakwera aliyeingia madarakani Juni mwaka huu akitokea chama cha upinzani, hii ni ziara yake ya kwanza nchini Tanzania na anaifanya wakati ambapo jirani yake Tanzania ikiwa katika vuguvugu la kuekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Tansania Offizieller Besuch des Präsidenten von Malawi in Tansania
Rais John Magufuli akifurahia jambo na mgeni wake, rais Lazarus Chakwera wa Malawi, baada ya Chakwera kuwasili jijini Dar es Salaam kwa ziara ya siku tatu, Oktoba 07, 2020.Picha: Department of information and communication of Tanzania

Mwenyeji wake, Rais Magufuli ambaye katika kipindi cha utawala wake wa miaka mitano, amezuru mara moja nchini Malawi amesema ni jambo la furaha kwake kumpokea mgeni hasa wakati huu anapojiandaa kuingia kwenye uchaguzi mkuu.

Soma zaidi: Rais Mteule wa Malawi Lazarus Chakwera ni nani?

'Urafiki wa chanda na pete'

Ameeleza kwamba Malawi na Tanzania ni marafiki wa chanda na pete na urafiki wao umesisiwa tangu wakati wa utawala wa kilononi na uhusiano huu umeendelea kuimarika hadi wakati huu ambako mataifa yote yamepindukia kipindi cha miaka 50 ya uhuru.

Viongozi hao walitarajiwa kuweka jiwe la msingi kwenye kituo cha mabasi cha Mbezi Luis nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kituo hicho kinachoendelea kujengwa, kinachokadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 22, sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 51, kitakuwa na basi za mikoani na nje ya nchi, zikiwemo zinazokwenda na kutoka Malawi, na kitakuwa na uwezo wa kushughulikia karibu mabasi 3,430 kwa siku.

Tansania Offizieller Besuch des Präsidenten von Malawi in Tansania
Rais Mgufuli akiwa katika mazungumzo na mwenzake wa Malawi, Lazarus Chakwera katika ikulu ya Dar es Salaam, Oktoba 07, 2020.Picha: Department of information and communication of Tanzania

Profesa Kabudi alisema ziara ya Chakwera ilifuatia mwaliko wa Rais Magufuli aliyoutuma baada ya ziara yake ya kiserikali nchini Malawi mwezi Aprili mwaka jana, wakati Peter Mutharika akiwa rais.

Soma zaidi: Uchaguzi Malawi mgombea wa upinzani aongoza matokeo ya awali

Bwana chakwera aliapishwa kuwa rais mwezi Juni mwaka huu, baada ya kushinda uchaguzi wa marudio katika uchaguzi uliobishaniwa. Ushindi wa Mutharika mwezi Mei 2019, ulibatilishwa mwezi Februari na mahakama ya katiba kuhusiana na madai ya udanganyifu.

Miradi ya pamoja

Tangu kungia madarakani, Rais Chakwera alifanya ziara za kikazi za siku moja nchini Zambia, Zimbabwe na Msumbiji, ambayo ni mataifa wanachama wa jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC.

Tanzania imekuwa nchi ya nne ya SADC ambayo kiongozi huyo wa Malawi ameitembelea, ambako alitarajiwa pia kuzuru bandari ya Dar Es Salaam na Kituo cha Mizigo ya Malawi, kinachoshughulikia mizigo inayoelekea katika taifa hilo lisilo na njia ya bahari.

Tansania Offizieller Besuch des Präsidenten von Malawi in Tansania
Rais Lazarus Chakwera akikagua gwaride la heshima baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kiserikali, Oktoba 07, 2020.Picha: Department of information and communication of Tanzania

Kwa mujibu wa waziri Kabudi, mataifa yanaendesha miradi ya pamoja ya miundombinu, miongoni mwake vituo vaa pamoja vya ukaguzi wa mpakani vilivyoko Songwe na Kasumulo, ukanda wa Mtwara, na pia katika bonde la Mto Songwe.

Ingawa mataifa haya jirani ambayo raia wake wanapatikana kwa wingi sehemu zote mbili, kuelezea namna yanavyokubaliana kwa mengi, hata hivyo kwa nyakati tofauti yamejikuta yakitumbukia katika mzozo kuhusu mpaka wa waziwa nyanya.

George Njogopa amechangia ripoti hii kutoka Dar es Salaam