1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yashughulikia adha za madereva wanaokwama mipakani

7 Mei 2020

Serikali ya Tanzania imesema imeanza kuzitafutia majibu changamoto zinazowakabili madereva wa nchi hiyo wanaosafirisha bidhaa katika mataifa jirani, ambao wamekuwa wakikabiliwa na vizingiti katika maeneo ya mipakani.

https://p.dw.com/p/3btFZ
Brasilien - Straßenblockade gegen hohe Treibstoffpreise
Picha: Getty Images/AFP/D. Magno

Kama sehemu za kuzitatua changamoto hizo zinazowaandamana madereva hasa wakati huu wa janga la corona, Tanzania imesema inaanzisha majadiliano ya mataifa jirani yanayotegemea bandari ya Dar es salaam kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao zinazoagizwa kutoka nje.

Hatua hiyo inakuja baada ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika, SADC, kuweka vizingiti kwenye maeneo ya mipakani, kama hatua ya kujihami na maambukizi ya virusi vya corona. Maderva hasa wale wa magari makubwa kama malori ndiyo waathirika wakubwa wa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na mataifa hayo.

Matumaini ya suluhisho kupitia mazungumzo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Kanali Wilbert Ibuge amesema anaamini kuwa kupitia majadiliano hayo, madhila yanayowakumba madereva hao yataondolewa.

China Jinggangshan Schiff in Tansania
Bandari ya Dar es Salaam inatumiwa na nchi nyingi majirani wa Tanzania zisizopakana na bahariPicha: imago/Xinhua/Z. Ping

 ''Majadiliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni na baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa SADC ambao waliridhia usafirishaji wa bidhaa muhimu wakati huu wa janga la corona.'' Amesema Balozi Ibuge.

Kwa muda wa wiki kadhaa sasa madereva wa Tanzania wamekuwa wakilalamika, wakisema wananyanyaswa katika maeneo ya mpaka wa Zambia. Tayari wizara ya mambo ya nje ya Tanzania imekutana na balozi wa Zambia nchini humo ili kujadili namna ya kuzitatua changamoto hizo.

Matatizo sio ukanda wa SADC tu

Kadhalika madereva wa Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu pindi wanaposafiri kuingia mataifa mengine kama vile Rwanda.

Wamesema wamekuwa wakilazimika kusimama muda mrefu, na wakati mwingine wakipigwa marufuku kuingia katika mataifa hayo jirani, wakishukiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona. Baadhi yao wamekuwa wakitakiwa kushusha mizigo mpakani.

Asilimia kubwa ya nchi jirani na Tanzania zimeongeza udhibiti katika maeneo ya mipakani na kuweka vizuizi kwa raia wake kutosafiri ovyo, kama hatua ya kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona wakati ambapo Tanzania imeendelea kuacha wazi mipaka yake.