Putin asema hajutii kuivamia Ukraine
28 Oktoba 2022Rais Vladimir Putin Ametoa kauli hiyo wakati mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu ya nishati yakisababisha katizo kubwa la umeme katika mji mkuu Kyiv na maeneo mengine.
Katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa mwaka kuhusiana na masuala ya sera za kigeni hapo jana mjini Moscow, Putin aliorodhesha kile kilichoonekana kama malalamiko dhidi ya wapinzani wao wa magharibi, akisema ubabe wa mataifa hayo mbele ya ulimwengu sasa unafikia tamati.
Soma Zaidi:Marekani yaonya kuhusu tishio la nyuklia la Urusi
Putin aliyatuhumu mataifa hayo ya magharibi kwa kuchochea vita vya nchini Ukraine na kucheza kile alichokitaja kama "mchezo mchafu" ambao umeibua balaa kubwa kote ulimwenguni. Akasema ni mataifa hayo sasa yanayowajibika kuzungumza na Urusi na mataifa mengine yenye nguvu kuhusiana na mustakabali wa ulimwengu.
"Tulijaribu kujenga uhusiano na nchi za Magharibi na NATO. Tulikuwa na ujumbe mmoja: tuache kuwa maadui, tuishi pamoja. Tufanye mazungumzo, tujenge ujasiri, ili tuwe na amani. Tulikuwa waaminifu kabisa.... nataka kusisitiza. Tulijua kabisa utata uliokuwepo kutokana na ukaribu kama huo. Lakini tuliamua kuchukua mkondo huo. Na majibu yake yalikuwa yapi? Tuliambiwa na NATO 'hapana', katika maeneo yote ya ushirikiano." alisema Putin.
Rais wa Marekani Joe Biden hata hivyo ametilia mashaka matamshi haya ya Putin, wakati taifa hilo likiandaa msaada mpya wa dola milioni 275 kwa ajili ya Ukraine ili kujiimarisha kimashambulizi dhidi ya vikosi vya Urusi,
Mzozo kati ya Urusi na Ukraine ulioanza miezi minane iliyopita umesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine mamilioni kuyakimbia makazi yao, lakini pia ukisababisha mtikisiko mkubwa wa uchumi wa ulimwengu na kufungua upya migawanyiko iliyoshuhudiwa enzi ya Vita Baridi.
Soma Zaidi: Vikosi vya Ukraine vyakabiliana na wanajeshi wa Urusi Donetsk
Rais Volodymyr Zelensky asema mashambulizi ya Urusi hayawakatishi tamaa.
Maafisa wanasema mashambulizi ya Urusi ambayo sasa yanalenga miundombinu ya nishati nchini Ukraine, yamesababisha katizo kubwa la umeme katika mji mkuu Kyiv na maeneo mengine.
Rais Volodymyr Zelensky amesema kwenye ujumbe kwa njia ya video jana usiku kwamba, mashambulizi hayo kamwe hayatawavunja moyo watu wa Ukraine. Kwenye video hiyo, Zelensky alikuwa amesimama nje, kwenye giza totoro, pembeni mwa ndege isiyokuwa na rubani ya Urusi iliyoangushwa na wanajeshi wa Ukraine.
Mapema leo, jeshi la Ukraine lilitoa kwa ufupi taarifa ya mikakati ya kijeshi katika jimbo la kusini mwa nchi hiyo la Kherson ambako wanajeshi wa Ukraine na Urusi wamekuwa wakijiandaa kwa wiki kadhaa sasa kwa kile kinachotarajiwa kuwa moja ya mapigano makali yanayoweza kushuhudiwa katika vita hivyo.
Vikosi vya Ukraine vimewaua wanajeshi 44 wa Urusi katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, hii ikiwa ni kulingana na chapisho kwenye mtandao wa Facebook wa jeshi la Ukraine, katika eneo la kusini mwa nchi hiyo. Wanajeshi hao walitumia risasi rashasha na makombora kushambulia ghala la silaha na vifaa vingine. Hata hivyo shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha taarifa hizi.
Mashirika: RTRE