Pande zinazopingana Syria kukutana , mazungumzo ya amani huenda yasifanyike
25 Januari 2014Katika hatua inayoonesha hali ya mambo itakavyokuwa hapo baadaye, duru za kidiplomasia zimesema siku mbili za mwanzo za mazungumzo hayo ya Geneva zitajumuisha kujadili makubaliano ya kuruhusu misaada kuingia katika mji mmoja , Homs, ambako watu hawana chakula.
Mkutano huo wa amani karibu uvunjike jana Ijumaa (24.01.2014), siku ambayo mazungumzo ya ana kwa ana yalikuwa yaanze, na yamerejea tena katika njia yake baada ya mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi kuzishawishi pande hizo mbili kulenga katika masuala madogo kwanza ambayo wanaweza kukubaliana.
Njia haitakuwa laini
"Tunatarajia njia yenye misukosuko," Brahimi amewaambia waandishi habari baada ya kufanya mikutano tofauti na pande hizo mbili.
Kukiwa na mgawanyiko kimataifa kuhusu jinsi ya kumaliza mzozo huo na kusababisha suluhisho la jumla la kisiasa kukosekana, pande hizo mbili zitalenga sasa katika masuala madogo, ujenzi wa uaminifu baina yao kukiwa hakuna uhakika iwapo majadiliano yanaweza hata kudumu kwa muda wa wiki moja.
"Pande zote mbili zitakuwa hapa kesho .... hawataondoka Jumamosi ama Jumapili," amesema Brahimi. Mjumbe wa upinzani Anas al-Abdah amesema kuwa hatua hizo zitaanza kwa mkutano mfupi leo Jumamosi ambapo ni Brahimi pekee atakayezungumza, utafuatiwa na mkutano mwingine mrefu mchana. Hata huo huenda usifanyike.
Duru moja ya kidiplomasia , ikidokeza mashambuliano makali ya maneno ambayo yalijitokeza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika mji wa Montreux nchini Uswisi siku ya Jumatano, amesema jana Ijumaa kuwa anachukua tahadhari sana.
Bora kidogo kuliko kukosa kabisa
"Ikilinganishwa na siku 10 zilizopita , tumekuwa mjini Montreux na ujumbe wa pande zote, tumeanza mkutano wa Geneva kwa uchelewesho wa siku moja zaidi, kesho dakika 30 pamoja na ujumbe wa pande hizo mbili na kisha huenda kuna jambo ambalo watakubaliana. Hatua ndogo, lakini hatua ndogo ni bora kuliko kukosa kabisa."
"Ni wazi kuwa kutakuwa na matukio ya miripuko kila siku katika mkutano huo."
Upatikanaji wa njia ya kuingiza misaada ya kiutu katika mji wa Homs, ambako waasi wamezingirwa katika wilaya ya kati na majeshi ya rais Bashar al-Assad, ni suala linaloweza kuafikiwa haraka.
"Hatua za kiutendaji zimekwisha shughulikiwa. Mambo yako tayari na iwapo serikali haitaweka vikwazo dhidi ya hatua hiyo inaweza kutokea haraka ," duru za kidiplomasia zimesema.
Wakati huo huo wataalamu wa masuala ya uhalifu wa kivita wa Umoja wa Mataifa wameweka pamoja taarifa za mateso na mauaji kutoka pande zote zinazohusika katika mzozo wa Syria na wana imani wanaweza kujenga kesi ambayo inaweza kuchukuliwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, mjumbe wa ngazi ya juu wa kikosi hicho amesema siku ya Ijumaa.
Wanatayarisha orodha ya nne ya siri , ama watu mmoja mmoja , ama vikundi vinavyohusika na uhalifu uliotokea tangu Julai, Karen koning AbuZayd, mtaalamu raia wa marekani anayefanyakazi katika tume huru ya uchunguzi iliyoundwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2011, amesema katika mahojiano.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani