1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa serikali ya Syria na Upinzani kukutana ana kwa ana

Mjahida24 Januari 2014

Serikali ya Syria na upinzani leo wanatarajiwa kukaa kwa mara ya kwanza katika meza moja ya mazungumzo kujadili namna ya kumaliza ghasia nchini humo zilizodumu kwa takriban miaka mitatu.

https://p.dw.com/p/1AwWs
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu Lakhdar BrahimiPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Pande hizo mbili zinazohasimiana zinatarajiwa kukutana leo katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ilioko Geneva, Uswisi, ambako mazungumzo yanaaminika kujikita katika suala la kuachiwa wafugwa na pia uwezekano wa kufungua njia kwenye miji na vijiji kwa wafanyakazi wa kutoa misaada.

Pande hizo mbili zilishambuliana waziwazi katika ufunguzi wa mazugumzo hayo siku ya Jumatano mjini Montreux.

Wawakilishi kutoka Damascus walitaka mkutano huo ujikite kujadili kitisho cha ugaidi kutoka kwa makundi yalio na itikadi kali yanayofanya kazi zao ndani ya Syria.

Wajumbe katika mkuano wa Syria mjini Montreux
Wajumbe katika mkuano wa Syria mjini MontreuxPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Lakini muungano wa kitaifa wa upinzani Syria ukataka majadiliano yaanze kwa kuzingatiwa kuundwa kwa serikali ya mpito, na kuondoka madarakani kwa rais Bashar Al Assad jambo ambalo utawala wa Assad umetupilia mbali.

Tofauti zaonekana kabla ya mkutano wa ana kwa ana kuanza

Aidha katika mkesha wa kuaza kwa mazungumzo ya leo, Mkuu wa muungano wa Upizani Ahmad Jarba ameutaja utawala wa Assad kuwa ni utawala unaokufa na uliokatili huku maafisa wa Syria wakitilia shaka uhalali wa muungano huo.

Imani ya kupatikana kwa hatua Licha ya hayo yote wajumbe wa upinzani wameendelea kuwa na imani kubwa kuwa hatua huenda ikapigwa katika kutafuta suluhu ya kumaliza ghasia ambazo hadi sasa zimesababisha mauaji ya watu 130,000.

Mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jaafari
Mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar JaafariPicha: Reuters

" Tunajua kuwa kuelekea njia ya makubaliano ya kisiasa ni ndefu lakini kila safari huanza kwa hatua ya kwanza," Alisema Mjumbe wa upinzani Burhan Ghalioun, alipokuwa na mazungumzo na shirika la habari la ujerumani- dpa.

Iwapo majadiliano ya siku mbili yanayoanza leo yataonesha dalili za mafanikio, wajumbe wa upinzani na wapatanishi watatarajia muda wa majadiliano kuongezwa hadi miezi sita, yakifanyika katika miji tofauti barani ulaya.

Aidha Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi, anayetarajiwa kukutana na pande zote mbili kwa muda tofauti hii leo kabla ya kuzishawishi kukutana ana kwa ana, jana alijadilli na pande hizo namna mazungumzo ya leo yatakavyofanyika.

Lakhdar Brahimi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.
Lakhdar Brahimi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Picha: Philippe Desmazes/AFP/Getty Images

Hata hivyo hakuna taarifa zaidi zilizotolewa juu ya mkutano wake na pande hizo mbili hasimu.

Matarajio ya kufanikiwa kwa mazungumzo hayo ni madogo sana, lakini wanadiplomasia wanaamini kwamba kuzileta pamoja pande hizo mbili kwa mara ya kwanza ni hatua ya mwanzo kabisa muhimu kujaribu kuleta upatanishi na kusitisha mapigano yaliowaacha raia wengi wa Syria bila makaazi.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman