Saud Arabia yapigania ushawishi Syria
24 Januari 2014Mustakbal wa Syria unapojadiliwa nchini Uswisi,miongoni mwa wajumbe mazungumzoni ni mwanamfalme wa Saudi Arabia Saud al Faisal.Kwasababu Saudi Arabia ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa makundi ya upinzani ya Syria.Mjini Montreux waliketi kwa mara ya kwanza tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe viliporipuka mapema mwaka 2011, wawakilishi wa serikali ya Bashar al Assad na wale wa upinzani .
Utawala wa mjini Riadh unataka vimalizike haraka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vinavyoihusu pia nchi hiyo ya kifalme.Vifaru,mitambo ya kujikinga dhidi ya makombora na bunduki ni miongoni mwa silaha wanazopatiwa wafuasi wa upande wa upinzani wa Syria kutoka Saudi Arabia.
Rasmi Inatajwa Silaha Hizo Zimelengwa Kuwafikia Wafuasi wa Jeshi Huru la Syria.
Lakini nchi hiyo ya kifalme tajiri kwa mafuta inatuma pia pesa:Wapiganaji wa jeshi huru la Syria wanapatiwa mshahara ,tena wanalipwa kwa sarafu ya Euro au dola.Kiwango cha mshahara huo ukilinganishwa na mshahara wa wastani nchini Syria,basi mtu anaweza kusema ni cha juu sana.Serikali mjini Riadh inataraji kwa namna hiyo kuwashawishi wanajeshi wengi zaidi wa serikali ya Assad watoroke jeshini.
Mbali na uungaji mkono huo,Saudi Arabia inajaribu pia kwa mlango wa nyuma kuimarisha ushawishi wake nchini Syria,anasema Anna Sunik.Mtaalam huyo wa masuala ya kisiasa anafanya uchunguzi katika taasisi ya taaluma jumla- na kieneo-GIGA mjini Hamburg-kitovu cha utafiti wake kikituwama katika nchi za kifalme za Ghuba la uajemi.
"Inadhaniwa na katika kadhia tofauti kuna ushahidi au taarifa rasmi zinazoonyesha kwamba Saudi Arabia inayaunga mkono pia makundi mengine ya waasi nchini Syria-mengi kati yao yanafuata msimamo wa kidini-yanawapatia wafuasi wake mazowezi na silaha."Anasema bibi Anna Sunik.
Zaidi ya hayo kuna ripoti zinazosema Saudi Arabia inawaachia raia wake kwenda kupigana nchini Syria.
Kuna sababu tofauti kwanini Saud Arabia inajihusisha sana na vita vya Syria.Sababu ya mwanzo kabisa ni Iran na sio Syria yenyewe.Nchini Syria,kila mmoja,Saudi Arabia na Iran anapigania ushawishi na usemi katika eneo hilo.
Mafahali Wawili Wapimana Nguvu
Ni mapigano ya kuania ushawishi,tangu wa kidini,kisiasa mpaka wa kiuchumi.Saudi Arabia na Iran, zinahasimiana tangu mapinduzi ya kiislam mnamo mwaka 1979.Watawala wa nchi hizo mbili wanajihalalisha kupitia madhehebu za kidini: Wale wanaoitwa Wahabi ambao ni Mkondo wa kihafidhina wa madhehebu ya Sunni- nchini Saudi Arabia na madhehebu ya Shia nchini Iran.
Syria lakini ni nchi yenye waumini wa dini na madhehebu tofauti.Wengi wa wakaazi wa nchi hiyo-asili mia 75 ni wa madhehebu ya Sunni-kuna waumini wa kikristo sawa na jamii za Druse na Alawi ambao ni waumini wa madhehebu ya Shia.
Ukoo wa Assad ni kutoka jamii ya Alawi. Na ndiyo maana Iran inahisi kuwa hiyo ni sababu ya kutosha kuiunga mkono Syria huku Saudi Arabia ikihisi kwa upande wake hiyo ni sababu ya kutosha kuupiga vita utawala wa Assad.
Lakini Iran inashawishiwa pia na umuhimu wa kijeografia wa Syria.Kupitia Syria,Iran inapata njia ya kuitumia bahari ya Mediterani kuwafikia Hisbollah nchini Libnan.
Wadadisi wanakubaliana hata kama kinyang'anyiro cha kupigania masilahi ya kisiasa ndio kipa umbele,hata hivyo nchini Syria,mafahali wawili wakubwa kiuchumi wanapimana nguvu:Saudi Arabia ina miliki shehena kubwa zaidi ya mafuta ulimwenguni na Iran inashikilia nafasi ya tatu.
Saud Arabia Kifua Mbele
Ingawa sekta ya mafuta ya Iran iliathirika kutokana na miaka kadhaa ya vikwazo vya kimataifa,lakini katika kongamano la kimataifa la kiuchumi mjini Davos rais Hassan Ruhani amebainisha kwa namna gani uhusiano wa kiuchumi na nchi za nje ni muhimu katika kuijenga upya nchi yake.Kwa Saudi Arabia hili ni pigo kuiona Iran inayoongozwa na Ruhani ikirejea tena katika jukwaa la kimataifa.
Hata hivyo inayoonyesha kuibuka na ushindi angalao kwa sasa ni Saudi Arabia baada ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon kufutilia mbali mwaliko wake kwa Iran katik duru ya pili ya mazungumzo ya amani ya Geneva kutokana na shinikizo la makundi ya upinzani ya Syria na nchi za magharibi.
Mwandishi:El Moussaoui,Najima/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman