Mkutano wa Geneva II waanza kwa mzozo
22 Januari 2014Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, aliufungua mkutano huo kwa kuzitolea wito pande zinazopingana nchini Syria kutumia fursa ya mkutano huu kutatua mgogoro wao, wakikumbuka kwamba Syria ni nchi yao wenyewe na kwamba wana mengi yanayounganisha.
"Bado Wasyria ni wamoja katika mapenzi yao makubwa kwa nchi yao, wana fahari ya urathi wao wa kitamaduni na kidini, na historia ya muda mrefu ya kuishi kwa amani. Wasyria wanapaswa kuzungumza tena ili kukirejesha kile ambacho kimewapotea. Ni muhimu kwamba Wasyria wote, wake kwa waume, washiriki katika jitihada za kuijenga nchi yao." Alisema Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewataka wawakilishi wa serikali na waasi ambao wanakutana kwa mara ya kwanza uso kwa uso baada ya mapigano kati yao kwisha kuwauwa zaidi ya watu 130,000 na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, kufanya kila wawezalo kurejesha amani kwenye nchi yao.
Urusi yataka Assad awe kwenye kipindi cha mpito
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambayo nchi yake ni mshirika muhimu wa serikali ya Bashar al-Assad, amewaambia wajumbe kutoka zaidi ya mataifa 40 na jumuiya za kimataifa waliokusanyika kwenye mkutano huo, kwamba kazi ya kuutafuta mkataba wa amani haitakuwa rahisi wala rahisi kiasi hicho, ingawa mkutano huo ni tukio kubwa la kihistoria.
Lavrov amesema washiriki wote wa mkutano huo wana wajibu wa kuhakikisha kuwa unafanikiwa, ili kumaliza kile alichokiita "mzozo wenye misiba" na kuuzuia kusambaa kwenye nchi nyengine katika eneo hilo.
Urusi inashikilia Rais Bashar al-Assad awemo kwenye kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.
Katika kauli inayoonekana kuwalenga waungaji mkono wa makundi ya waasi, Lavrov ameuambia mkutano huo kwamba "wachezaji wa nje" hawapaswi kujiingiza kwenye mambo ya ndani ya Syria, ingawa alikosoa kutokuwapo kwa Iran kwenye mkutano huo, akisema taifa hilo ambalo pia ni muungaji mkono wa utawala wa Assad, lazima liwe sehemu ya mdahalo wa kimataifa juu ya Syria.
Marekani yapinga Assad kuwamo
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ambaye alizungumza baada ya Lavrov, alionesha wazi kutokubaliana na pendekezo la Rais Assad kuwa sehemu ya utawala wa mpito, ambao ni kati ya ajenda muhimu za mkutano huu.
Kerry amesisitiza kwamba ni lazima Assad aondoke madarakani, huku akikumbushia kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria visingalikuwapo endapo pale lilipoanza vuguvugu dogo la wanafunzi mjini Dara'a miaka mitatu iliyopita, serikali ya Assad ingeliwasikiliza watoto hao.
"Kilichokosekana kwenye ripoti za kila siku za ghasia hizi ni ukweli kwamba mapinduzi haya hayakuanza kama vita vya silaha. Yalianza kwa amani. Yalianzishwa na watoto wa skuli mjini Dara'a waliokuwa tu na mikebe ya kupaka rangi, ambao waliandamana kwa amani kudai mageuzi. Wakakabiliwa kwa fujo na wazazi wao walipojitokeza kulalamikia kukamatwa kwa watoto wao, watu 120 waliuawa. Hapo ndipo yalipoanza." Amesema Kerry.
Muallem aja juu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid Muallem, ambaye ilibidi akatishwe na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye hotuba yake refu, alifika umbali wa kuwalaumu waungaji mkono wa wapinzani kwamba wana damu mikononi mwao, kwa kuwapa silaha na mbinu za mauaji ndani ya ardhi ya Syria.
Muallem amewakosoa pia wapinzani kwa kuwa wasaliti na mawakala wa Israel, wakilenga kulibomoa taifa lao, huku akizisifu Urusi, Iran na baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini, Arabuni na Afrika kwa kutokukubali kile alichokiita uzushi wa magaidi.
Kiongozi wa upinzani, Ahmad Jarba, alikumbushia mauaji ya watoto wadogo mjini Dara'a kuwa ndio msingi wa vuguvugu la uasi dhidi ya serikali. Jarba ameuambia mkutano kuwa vita nchini Syria, ambavyo hadi sasa vimeshauwa watoto 10,000, vimetawaliwa na taarifa za upotoshaji kutoka upande wa serikali.
Hadi tunakwenda hewani, wakati mkutano ukiendelea, siku hii ya kwanza inaweza kutajwa kama siku ya kutoa joto la ndani kwa kila upande kwenye mzozo huu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo