Nigeria kuwaadhibu waliohusika na mashambulizi ya droni
8 Desemba 2023Makamu wa Rais Kashim Shettima amekiambia kituo cha televisheni cha nchini humo wakati alipowatembelea majeruhi waliolazwa kwenye mji wa Kaduna kwamba serikali itachunguza na kuwaadhibu wahusika wote na wahanga wa shambulizi hilo watasaidiwa.
Rais Bola Tinubu tayari aliagiza kufanyika uchunguzi wa kisa hicho.
Soma zaidi: Rais Nigeria Bola Tinubu aamuru uchunguzi baada jeshi kuwaua watu 85
Jeshi limejitetea kwa kusema lilitafsiri tofauti shughuli iliyokuwa ikifanywa na kundi la watu ambalo waliliona wakati wa doria ya angani, kwenye jimbo la Kaduna, kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuongeza kuwa waliwafananisha na majambazi.
Droni hiyo iliwaua watu kwenye kijiji cha Tudun Biri, ambapo watu walikuwa wakisherehekea sherehe ya Kiislamu.
Duru rasmi zilisema watu 85 walikufa na 66 walijeruhiwa.
Shirika la Kimataifa la haki za Binaadamu la Amnesty International limesema watu 120 waliuawa.