1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo Israel- Hamas utaathiri vipi mkutano wa COP28?

28 Novemba 2023

Mazungumzo katika mkutano wa kila mwaka wa hali ya hewa yamekuwa magumu kila wakati. Wachunguzi wa mambo wanasema mzozo unaoendelea, ambao unaleta mgawanyiko kwa mataifa ulimwenguni, unaweza kufanya mambo kuwa magumu.

https://p.dw.com/p/4ZXJX
COP28 Dubai | Ukumbi ambao utafanyika mkutano wa kilele wa COP28
Watu wakitembea nje ya ukumbi ambao utafanyika mkutano wa kilele wa COP28 dubaiPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Wakati mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa ukikaribia, mzozo wa Israel na Hamas huko Gaza unaibua changamoto.

Waangalizi wanakadiria kwamba  mzozo huo utaathiri ushirikiano wa kikanda na mustakabali wa sera za mazingira za Mashariki ya Kati. 

Mwaka jana, mradi uliosifiwa sana wa nishati ya kiikolojia ulioshirikisha na mahasimu wa zamani Jordan na Israel ulipendekezwa kama mfano wa jinsi sera rafiki kwa mazingira zinaweza kuleta mustakabali bora katika Mashariki ya Kati.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck, alisifu mradi huo unaojulikana kama "maji kwa nishati", akisema iwapo utafanyika kama ilivyopangwa, itakuwa ni mfano mzuri wa jinsi mataifa ya Kiarabu yalivyokuwa yakishirikiana na Israel na kwamba "itajenga uaminifu na kuwa msukumo wa ushirikiano badala ya makabiliano."

Soma pia:Joto kali kusababisha vifo zaidi kufikia 2050

Lakini kufikia sasa matumaini ya mradi huo ambao ulitakiwa kuiona Jordan ikiipatia Israel nishati ya jua na Israel kupeleka maji yaliyosafishwa kuondoa chumvi Jordan  yanaonekana kupotea kabisa.

Makubaliano hayo yalikubaliwa mwezi Novemba mwaka jana na yalipaswa kutiwa saini katika mkutano wa hali ya hewa COP28 mwezi huu wa Novemba katika  Umoja wa Falme za Kiarabu.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi katika mahojiano ya televisheni alisema hawatatia saini mkataba huo tena.

Safadi aliongezea kusema kwamba itakuwa vigumu kwa waziri wa Jordan kuketi karibu na waziri wa Israel kutia saini mkataba wa maji na umeme, wakati Israel inaendelea kuua watoto huko Gaza.

COP28 ni jukwaa la usawa kwa mataifa pinzani?

Mzozo unaoendelea kati ya Isreal na Hamas unaweza tu kuwa mfano wa kwanza wa uharibifu wa makubaliano katika mkutano wa COP28.

COP28 inachukuliwa kuwa mojawapo ya mikutano muhimu zaidi ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kwa sababu inaleta pamoja pande zote za Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Hili ni toleo la 28 na linafanyika Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwezi huu.

Dubai | Mtu akitembea katika nembo ya COP28
Mtu akitembea katika nembo ya COP28Picha: Amr Alfiky/REUTERS

Lakini kama makubaliano ya Israel na Jordan yanavyoonyesha, wapatanishi wanaohudhuria COP28 watalazimika kukabiliana na angalau baadhi ya athari za mzozo wa sasa kati ya Hamas na Israel.

Soma pia:Guterres atoa wito kuongeza juhudi kukabiliana na tabia nchi

Waangalizi wa mambo wanapendekeza kuwa kuna njia kadhaa ambazo mzozo wa Israel na Hamas, unaoendelea tangu shambulio la Oktoba 7 kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Hamas, unaweza kuathiri mazungumzo ya COP28, kwa njia thabiti na za muda mfupi.

Mkutano wa COP28 mwaka huu unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi na hali ya usalama inaweza kuwa hofu kwa baadhi ya wajumbe wapatao 70,000 wanaotarajiwa Dubai, huku kukiwa na hisia kali zinazosababishwa na mzozo huo katika Mashariki ya Kati.

Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ni utawala wa kifalme, kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International, hauruhusu maandamano yasiyoidhinishwa au dhidi ya serikali, haijashuhudia maandamano ya kupinga Israeli kama mataifa mengine katika eneo hilo.

Wala hakuna nchi zilizotoa tahadhari ya usafiri au maonyo kuhusu kwenda Dubai.

Hata hivyo bado kuna wasiwasi, Baadhi ya makampuni kwa mfano, benki ya Uswizi ya UBS mapema mwezi wa Novemba,  ilionya wafanyakazi dhidi ya usafiri wa kibiashara kwenda Mashariki ya Kati.

Wasiwasi kama Netanyahu atahudhuria COP28

Israel ilipanga kutuma takriban wajumbe 1,000 huko Dubai. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia alikuwa amealikwa kuhudhuria na anatarajiwa kufanya ziara huko Dubai mapema Desemba.

Israel Tel Aviv 2023 | Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Abir Sultan/AP Photo/picture alliance

Baadhi ya ripoti sasa zinasema kuwa wajumbe hao watapunguzwa. DW iliuliza wizara ya mazingira ya Israel kama nchi hiyo bado ina mpango wa kutuma wajumbe wengi na wanasiasa wakuu kwenye mkutao wa COP28 lakini wizara hiyo haikujibu.

Kunaweza kuwa na maandamano wakati wa mkutano huo lakini Umoja wa Falme za Kiarabu umesema utaruhusu maandamano, ambayo kwa mujibu wa Frederic Wehrey, mtaalamu katika Mpango wa Mashariki ya Kati katika Wakfu wa Carnegie kuhusu Amani ya Kimataifa, maandamano hayo bila shaka yataibua suala la hali mbaya ya Gaza, na jinsi uvamizi unaoongezeka wa Israeli, na uharibifu wake wa miundombinu na huduma za maji na uhamishaji mkubwa, utakuwa na athari mbaya na kubwa kwa Palestina ambayo tayari iko katika hali mbaya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Soma pia:Biden kutohudhuria Mkutano wa kilele wa COP28

Wataalam wanahoji kwamba ufadhili wa mipambano dhidi ya hali ya hewa pia unaweza kuathiriwa, Ikiwa mzozo huo utaendelea au kuenea, utakuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia.

Shirika la Fedha la Kimataifa ambalo linaakisi ni kiasi gani cha fedha kinachopatikana ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi mataifa yanavyohisi juu ya fidia ya kifedha na uchafuzi zaidi wa mazingira kwa nchi maskini na zilizoendelea kidogo.

Athari nyingine isiyoonekana sana inaweza kuakisiwa katika mitazamo ya nchi mbalimbali linapokuja suala la kukubaliana na mikataba kuhusu ulinzi wa mazingira.

Imependekezwa kuwa baadhi ya wanadiplomasia wakuu ambao kwa kawaida hujitayarisha kwa mazungumzo katika COP28 ambayo mara nyingi ni wakati mikataba inakamilishwa, badala ya kujadiliwa kwa maelezo ya kiufundi watavurugwa na mzozo huo.

Inawezekana pia kwamba wanadiplomasia kutoka nchi fulani wanaweza pia kutokuwa tayari kuafikiana na wengine sasa kwa sababu wanasimama pande tofauti za mzozo.

Ujerumani yaahidi euro bilioni mbili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi