Joto kali kusababisha vifo zaidi kufikia 2050
15 Novemba 2023Ripoti iliyotolewa na timu ya wataalam na kuchapishwa katika jarida la Lancet, inatabiri kuwa ongezeko la joto duniani litawaua watu, karibu mara tano zaidi ifikapo mwaka 2050.
Tathmini kuu ya kila mwaka inayofanywa na watafiti wakuu na taasisi, imeonya kuwa afya ya binadamu iko hatarini, ikiwa hatua mathubuti za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hazitochukuliwa.
Watafiti hao wameonya kwamba mamilioni ya watu watakabiliwa na Ukame zaidi utakaosababisha baa kubwa la njaa. Aidha pia, utafiti huo umebainisha kuwa magonjwa ya kuambukiza yanayoenezwa na mbu yataendelea kuenea katika maeneo mapya. Soma habari inayohusiana na hilo: Hali mbaya ya hewa inasababisha pia maradhi kwa watoto na hata wazee kutokana na ongezeko la joto ama baridi kali
Ripoti hiyo imetolewa kuelekea mazungumzo ya kimataifa ya mazingira ya COP28 yatakayofanyika Dubai baadae mwezi huu. Kulingana na utafiti wa jarida la Lancet, mnamo mwaka jana watu duniani kote walikabiliwa na wastani wa siku 86 za joto kali.