Muda wa usitishaji vita kati ya Israel na Hamas kuefushwa?
27 Novemba 2023Siku hizo nne zinamalizika usiku wa Jumatatu kwa majira ya nchini humo. Misri, Qatar, Marekani, Uhispania na Umoja wa Ulaya zinafanya juhudi za kuongezwa kwa muda huo.
Shirika la habari la AFP, limesema Hamas imewaarifu wasuluhishi kwenye mzozo huo kwamba wako tayari kuongeza muda wa kusimaisha mapigano kwa siku mbili hadi nne.
Soma zaidi: Mapatano kati ya Israel na Hamas yaingia siku ya mwisho
Israel hapo kabla ilisema ingeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa sharti la kuachiliwa mateka kumi, kwa kila siku moja ya ziada ya kusimamisha mapigano. Mapema hii leo, msemaji wa serikali ya Israel, Eylon Levy pia alisema kuna uwezekano wa kuongeza muda. Amesema wanataka kupokea mateka wengine 50 baada ya Jumatatu, ili kuwarejesha mateka wote nyumbani.
Mapema viongozi kadhaa wa kimataifa walitoa wito kwa Israel na kundi la Hamas kuongeza muda wa usitishaji vita ili kuruhusu misaada zaidi ya kiutu kuingia katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wanaozuiwa katika ukanda huo. Wito huo umetolewa wakati viongozi hao wakikutana huko Barcelona nchini Uhispania kujadili mzozo huo.
Borell: Kusitishwa mapigano kutaruhusu misaada Gaza
Katika mkutano huohuo Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, pia alisema kuwa anatumai mapigano yatasitishwa kwa muda mrefu zaidi katika Ukanda wa Gaza ili kuifanya hatua hiyo kuwa endelevu wakati kukitafutwa suluhisho la kisiasa.
Naye katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO amesema kuwa kurefushwa kwa makubaliano hayo kutaruhusu misaada inayohitajika sana na watu wa Gaza na kuitolea wito Iran kuwadhibiti mawakala wake. Tehran inafahamika kwa kuyaunga mkono makundi yanayoipinga Israel yakiwemo Hamas, Hezbollah na waaasi wa Kihuthi wa Yemen.
Katika hatua nyingine Rais wa Ujerumani, Frank -Walter Steinmeier amesema bunge la nchi yake limetenga kiasi cha dola milioni 7.6 kwa ajili ya kulifanyia ukarabati katika jumba la sanaa la jamii lililoharibiwa na shambulizi la Hamas.
Steinmeier ameitembelea jumuiya ya Be'eri ambayo ni moja ya jamii zilizoshambuliwa akiwa na rais wa Israel Isaac Herzog katika shambulio hilo la kushtukiza la Oktoba 7 kusini mwa Israel ambapo watu 1,200 waliuwawa.
Na katika hatua nyingine bilionea na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X Elon Musk, ambaye jukwaa lake hilo limekuwa likituhumiwa kwa matamshi ya chuki dhidi ya Wayahudi hii leo amelitembelea eneo la Israel lililoshambuliwa mwezi uliopita na Hamas, akiambatana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, wakati pia akitarajiwa kukutana na viongozi wakuu nchini humo.