Mgomo wa wafanyakazi wa JKIA-Kenya wamalizika
11 Septemba 2024Chama cha wafanyakazi wa mamlaka ya safari za ndege kimeridhia kuumaliza mgomo na kurudi kazini baada ya mgomo wa siku nzima uliosababisha kukwama kwa shughuli za safari za ndege katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Nairobi wa JKIA.
Hatua hiyo imetangazwa na katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi nchini Kenya, COTU, Francis Atwoli ambaye amesema wafanyakazi wa mamlaka ya safari za ndege na serikali wamekubaliana juu ya kusitishwa kwa mgomo huo.
Kuanzia usiku wa kuamkia leo shughuli zilikwama katika uwanja huo huku wasafiri wakibakia hawana la kufanya baada ya safari nyingi kufutwa na kucheleweshwa. Wafanyakazi wa JKIA walianzisha mgomo huo wakiishinikiza serikali iufute mpango wa kuipatia kampuni ya Adani kutoka India mamlaka ya kudhibiti uendeshaji wa uwanja huo kwa miaka 30.
Mgomo wa siku nzima
Mamia ya wafanyakazi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi JKIA wamegoma wakiupinga mkataba kati ya serikali na mwekezaji wa kigeni. Ndege nyingi zimeahirisha safari na kufanya mamia ya abiria kukwama uwanjani hapo.
Serikali imesema mkataba wa ujenzi na uendeshaji uliofikiwa na kampuni ya Adani ya nchini ndia ungeshuhudia ukarabati wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na upanuzi zaidi wa njia za kuruka na kutua ndege, kwa makubaliano ya kampuni hiyo kuuendesha uwanja huo kwa miaka 30.Mgomo wa wafanyakazi wavuruga safari za ndege Nairobi
Chama cha wafanyakazi wa viwanja vya ndege vya Kenya, kilichoitisha mgomo huo, kilisema kuwa makubaliano hayo yatasababisha upotevu wa ajira na huduma duni kwa wale watakaobaki.
Shirika la ndege la Kenya Airways mnamo siku ya Jumatano lilitangaza uwezekano wa kuchelewa ama kuahirishwa kwa safari za ndege kwa sababu ya mgomo unaoendelea katika uwanja huo.
Wiki iliyopita, wafanyakazi wa uwanja wa ndege walitishia kugoma, lakini mipango hiyo ilisitishwa ili kusubiri majadiliano na serikali. Muungano huo ulisema mgomo huo utaendelea hadi serikali ifutilie mbali mpango wa kukodisha uwanja wa ndege kwa kampuni ya Adani Group ya India kwa miaka 30 badala ya uwekezaji wa dola bilioni 1.85.Kenya Airways kuruka moja kwa moja hadi Marekani
Ada za mizigo na abiria kutoka uwanja wa ndege huchangia zaidi ya asilimia tano ya Pato la Taifa la Kenya.
Chama cha wanasheria nchini Kenya pamoja na tume ya haki za binadamu walifanikiwa kuishawishi mahakama kuu nchini humo, kuusimamisha kwa muda mpango huo kwa hoja kwamba makubaliano hayo hayakuwa wazi.