Wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa JKIA nchini Kenya wagoma
11 Septemba 2024Mgomo wa wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, mjini Nairobi, umesababisha safari za ndege za kuingia na kutoka Kenya kucheleweshwa na nyingine kufutwa kabisa. Hayo yameelezwa leo Jumatano na shirika la ndege la Kenya Airways.
Duru zimeliarifu shirika la habari la AFP kwamba shughuli zilisimama katika uwanja wa ndege wa JKIA leo Jumatano kufuatia mgomo wa wafanyakazi huku usimamizi wa uwanja huo ukitarajiwa kutowa taarifa.Ahmeda Abdulrahman ni miongoni mwa wasafiri waliokwama kwenye uwanja huo. Mmoja wa abiria aliyekwama Ahmeda Abdulrahman ameeleza kuwa; "ndege yetu ilipangwa kuondoka 6.45 asubuhi tumefika hapa saa kumi alfajiri. Tumekaa tukisubiri kwa masaa 6.Kimsingi toka wakati huo tumekaa tuu hatufanyi lolote,tumechoka na inasikitisha sana."
Wafanyakazi wa JKIA wanapinga mpango wa kuukodisha uwanja huo kwa kampuni ya Adani kwa kipindi cha miaka 30, kwa kuwekeza dola bilioni 1.85 nchini Kenya.
Wakosoaji wanasema mpango huo utasababisha upoteaji wa nafasi za ajira kwa wafanyakazi wa ndani na kuwapora walipa kodi, faida inayotokana na uwanja huo.
Serikali ya Kenya imeutetea mpango wake huo kwa kusema ni muhimu kwa ajili ya kuukarabati uwanja huo wa ndege wa Kimataifa. Chama cha wanasheria Kenya na tume ya haki za binadamu nchini humo walifanikiwa kuishawishi mahakama kuu nchini humo, kuusimamisha kwa muda mpango huo kwa hoja kwamba makubaliano hayo yamekosa uwazi.