Rigathi Gachagua amshutumu bosi wake Ruto kwa ukatili
20 Oktoba 2024Makamu wa Rais wa Kenya aliyeng'olewa madarakani, Rigathi Gachagua,Jumapili alimshutumu vikali bosi wake, William Ruto, kuwa katili mkubwa, akionya kwamba maisha yake yanaweza kuwa hatarini.
Gachagua aliondolewa madarakani na Seneti kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake Alhamisi, lakini agizo la mahakama limesitisha mchakato wa kumteua mrithi wake.
"Nimeshtushwa na jinsi mtu niliyemsaidia kuwa rais, niliyekuwa na imani naye, na nilieteswa kwa kumsaidia, anavyoweza kuwa na ukatili mkubwa dhidi yangu," aliwaambia waandishi wa habari.
Gachagua mwenye umri wa miaka 59, aliyekumbwa na mzozo, alisema ulinzi wake umeondolewa na wafanyakazi wake wote wamepewa likizo ya lazima.
Amwajibisha Ruto kwa lolote litakalomtokea
"Ikitokea chochote kwangu au kwa familia yangu, Rais William Ruto lazima awajibishwe," alisema, akidai kuwa kumekuwa na majaribio ya awali ya kumuua.
Alikuwa akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali katika jiji kuu la Nairobi, ambako alikuwa akipatiwa matibabu kwa maumivu makali ya kifua.
Soma pia: Ruto amteua Kindiki kuwa naibu mpya wa rais wa Kenya
Gachagua aliugua Alhamisi, takriban saa moja kabla ya kutoa ushahidi katika kesi ya kihistoria ya siku mbili ya kumng'oa madarakani.
Baraza la juu la bunge liliendelea na upigaji kura wa kumwondoa ofisini baada ya mawakili wake kushindwa kuahirisha kikao hicho.
Alipatikana na hatia kwa mashtaka ikiwa ni pamoja na kutishia majaji na kueneza siasa za mgawanyiko wa kikabila, lakini alisafishwa kwenye mashtaka ya ufisadi na utakatishaji fedha.
Uchaguzi wa Mrithi na Hatua za Mahakama
Katika sakata hiyo ya kisiasa inayobadilika kwa kasi, Ruto alimteua mara moja Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, kuchukua nafasi ya Gachagua.
Hata hivyo, Mahakama Kuu katika mji mkuu ilisitisha mchakato wa uteuzi huo dakika chache baada ya bunge kupiga kura kwa wingi kumuidhinisha Kindiki, msomi mwenye umri wa miaka 52 aliyebadilika na kuwa kiongozi mashuhuri wa kisiasa.
Jopo la majaji watatu linasubiri kusikiliza kesi hiyo Jumanne.
Soma pia: Kindiki: Msomi mnyenyekevu aliyegeuka kuwa kigogo wa kisiasa
"Rais, kwa kukiuka kabisa agizo la mahakama, ameondoa ulinzi wangu kwa ukatili," alisema Gachagua, licha ya yeye bado kuwa makamu wa rais.
"Sielewi ukatili wa aina hii... wakati mtu akiwa kwenye hali ya chini kabisa maishani na akijitahidi kwa kila hali kuendelea kuishi, unamfanyia ukatili mkubwa kama huo."
Ruto bado hajatoa tamko lolote hadharani kuhusu kumwondoa Gachagua madarakani.
Gachagua ni makamu wa rais wa kwanza kuondolewa madarakani kwa njia hii tangu kuanzishwa kwa sheria ya kumwondoa madarakani katika katiba mpya ya Kenya ya mwaka 2010.