Kindiki: Msomi mnyenyekevu aliyegeuka kuwa kigogo wa kisiasa
18 Oktoba 2024Milionea huyu mwenye umri wa miaka 52, ambaye amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya Ruto kwa zaidi ya miaka miwili, aliteuliwa kushika nafasi ya Naibu Rais siku ya Ijumaa, baada ya kufutwa kazi kihistoria kwa Rigathi Gachagua.
Ingawa anasifiwa na wafuasi wake kwa kuwa na urafiki wa kawaida na watu, profesa huyu wa sheria mwenye sauti ya upole amekumbwa na lawama hivi karibuni kutokana na madai ya ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoitikisa Kenya mapema mwaka huu.
Pia amekabiliwa na uchunguzi kuhusiana na utajiri wake wa dola milioni 5.4, ambao aliliambia bunge kuwa umetokana zaidi na kampuni yake ya uwakili na biashara ndogo ndogo.
Mwaka 2011, Kindiki alichaguliwa na Ruto, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa upinzani, kujiunga na timu yake ya kisheria kupinga mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika ICC.
Ruto alikabiliwa na mashtaka matatu — mauaji, kuwafurusha watu kwa nguvu, na mateso — kuhusiana na vurugu za kikabila baada ya uchaguzi wa 2007-2008 ambazo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100 na kuwafurusha makwao watu 600,000.
Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, ambaye pia alishtakiwa na ICC kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo, aliungana na Ruto kama mgombea mwenza wake na kushinda urais mwaka 2013. Kesi dhidi ya viongozi hao wawili hatimaye zilisambaratika kutokana na kile upande wa mashtaka ulisema ni kampeni ya mara kwa mara ya vitisho kwa mashahidi.
Mwanzo mgumu
Akiwa mtoto wa mhubiri katika kijiji cha Irunduni, eneo lenye wapiga kura wengi la Mlima Kenya, Kindiki ni mmoja wa watoto tisa, ambao wote wako katika taaluma au utafiti. Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Moi, Kenya, kabla ya kupata shahada ya uzamili na PhD kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini.
Soma pia: Gachagua atimuliwa wakati akiugua hospitali
Kindiki alifundisha sheria katika vyuo vikuu vya Kenya, na alipanda cheo hadi kuwa Naibu Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi, taasisi kuu ya elimu nchini.
Mwaka 2008, baada ya vurugu za uchaguzi, alijiunga na serikali kama katibu wa mshikamano wa kitaifa chini ya wizara ya haki ya wakati huo. Lakini alihudumu kwa siku 100 pekee kabla ya kurejea darasani, hadi alipohusika katika kesi ya ICC.
Kindiki alichaguliwa kuwa seneta wa Kaunti yake ya nyumbani ya Tharaka Nithi katika uchaguzi wa 2013, nafasi aliyoshinda tena mwaka 2017. Lakini alikuwa miongoni mwa waathirika wa kwanza wa mzozo kati ya Kenyatta na Ruto kuelekea uchaguzi wa 2022. Aliondolewa kama Naibu Spika wa Seneti katika harakati za Jubilee, chama cha Kenyatta, kupiga marufuku wafuasi wa Ruto bungeni.
Ndoto iliyotimia
Wafuasi wake wanamwona baba huyu wa watoto watatu kama kiongozi mnyenyekevu, akibebwa na taswira yake ya kuwa kiongozi wa umoja katika nchi yenye historia ya siasa za kikabila zenye vurugu. Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema hana uwezo wa kuwavutia umati kama Gachagua, ambaye hakuwa maarufu kitaifa kabla ya kuwa Naibu wa Ruto.
Wengi walitarajia Ruto angemteua Kindiki kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi wa 2022, lakini Gachagua aliibuka mshindi baada ya mkutano wa saa 17 kati ya muungano wa Kenya Kwanza uliokuwa ukitawala.
Soma pia:Mahakama Kuu Kenya yasimamisha mchakato wa kumtoa Gachagua
Ruto alikuja kumzawadia Kindiki, ambaye alisitisha azma yake ya kugombea tena useneta kwa matumaini ya kushinda nafasi ya Naibu Rais, kwa kumpa wadhifa muhimu wa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kindiki alikabiliwa na hasira ya umma alipotetea vitendo vya polisi dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano makubwa ya vijana yaliyofanyika mwezi Juni. Takriban watu 60 waliuawa, huku makundi ya haki za binadamu yakilaumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Ili kujaribu kutuliza maandamano, Ruto alimuondoa Kindiki mwezi Julai pamoja na karibu mawaziri wake wote, lakini akamteua tena haraka katika baraza jipya la mawaziri.