1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneti ya Kenya kupiga kura kuamua hatma ya Gachagua

17 Oktoba 2024

Naibu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua anasubiri kuijua hatma yake wakati maseneta wanajiandaa kupiga kura mintarafu mashtaka 11 yanayomuandama.

https://p.dw.com/p/4ltrq
Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua
Naibu rais wa Kenya Rigathi GachaguaPicha: picture alliance / NurPhoto

Naibu Rais Rigathi Gachagua atapata fursa ya kujitetea mbele ya Baraza la Seneti. Mashtaka hayo yanayomuandama ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, ufisadi na kukiuka katiba.

Kikao cha Baraza la Seneti kimeingia siku yake ya pili na ya mwisho ambapo maseneta watapata nafasi ya kuiamua hatma ya naibu wa rais Rigathi Gachagua. Usiku wa kuamkia leo, maseneta na mawakili wa pande zote walikwaruzana wakati wa kuwasilisha ushahidi na kutoa ufafanuzi.

Kikao hicho kiliendelea hadi saa sita usiku na hii leo Gachagua anatazamiwa kupanda jukwaani kujitetea. Hoja muhimu zilizoibuka ni madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ambayo huenda yakaibadili taswira ya kesi yenyewe.

Hii leo mambo yalichemka pale madai yalipotolewa kuwa naibu wa rais alimhadaa kaka yake, marehemu Nderitu Gachagua wakati alipokuwa anaugua ili atie saini wasia wake kabla ya kukata roho. Seneta wa Bungoma David Wafula alihoji suala la uhusiano.

Unaweza pia kusoma: Mahakama Kenya yakataa kuzuia kura ya seneti kuhusu kumng'oa madarakani naibu wa rais

Unaweza pia kusoma: Baraza la Seneti laanza kujadili hoja ya kuondolewa Gachagua

Kwa upande wake Spika wa Baraza la Seneti Amason Kingi, aliruhusu ushahidi uliokuwa umewasilishwa kutumika ambao ulimuweka pabaya naibu wa rais aliyetuhumiwa kwa kutumia mtu wa kando kununua hoteli ya kifahari iliyokuwa inamilikiwa na marehemu Nderity Gachagua, hatua iliyozua mjadala mkali barazani.

Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse aliyewasilisha mswada huo bungeni kwa mara ya kwanza alikuwa na kibarua kigumu kujibu maswali yaliyoulizwa na wakili wa naibu wa rais Elisha Ongoya.

Unaweza pia kusoma: Gachagua akanusha madai ya ufisadi na kujilimbikizia mali

Mutuse aliyelazimika kutoa ufafanuzi anamtuhumu Rigathi Gachagua kwa kujilimbikizia mali yenye thamani ya shilingi bilioni 5.2 za Kenya, tangu alipoingia madarakani. Wakili Ongoya alitaka kujua alikozitoa takwimu hizo ukizingatia taaluma yake.

Kenya Nairobi | William Ruto na Rigathi Gachagua
Rais William Ruto hajatoa kauli yoyote ya moja kwa moja kuhusu masaibu na mchakato wa kumuondoa naibu wake madarakani.Picha: Simon Maina/AFP

Mbali na madai hayo ya kujilimbikizia mali kwa njia zisizokuwa sawa, Mbunge wa Kibwezi Mashariki kadhalika alisukumwa kutoa ushahidi kuwa naibu wa rais Gachagua alitumia watu wa kando kujipatia kandarasi ya vyandarua vya mbu vilivyotiwa dawa vya thamani ya shilingi bilioni 3.7 za Kenya kupitia mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za tiba, KEMSA.

Unaweza kusoma pia: Bunge la Kenya lapiga kura kumuondoa madarakani Gachagua

Kulingana na muswada huo, naibu wa rais aliwashinikiza viongozi wa KEMSA kumpa kandarasi hiyo ya vyandarua vya mbu kutumia kampuni ya Crystal Ltd kinyume na utaratibu jambo ambalo halijathibitika. Seneta wa Mombasa Mwinyi Haji Fakii alikuwa na haya ya kuuliza kuhusu kashfa ya KEMSA.

Hoja nyengine iliyoibuka ni kuwa naibu wa rais amekuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa Wakenya wananufaika kwa kuzingatia mchango wao wa kisiasa kupitia vyama jambo ambalo limewakasirisha wengi. Hata hivyo, wakili wa Gachagua, Elisha Ongoya alifafanua kuwa katika mazingira ya muungano wa vyama, hilo haliepukiki.

Mchakato huu inajikita pia katika suala la naibu wa rais kujilimbikizia mali kama vile hoteli ya kifahari ya Outspan, Olive Gardens na Treetops kwa kasi, hali inayoashiria kuwa kuna mkono wa ufisadi.

Shughuli itakamilika baada ya saa mbili usiku pindi maseneta watakapopiga kura itakayoiamua hatma ya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua. Ili atimuliwe, maseneta wasiopungua 45 ambao ni sawa na thuluthi mbili wanahitaji kupiga kura ya kumuondoa mdarakani. Endapo atasalimika ataendelea kuhudumu na kupambana.