Mafuriko Kongo yaendelea kuathiri wakaazi
29 Desemba 2023Shirika linahusika na usimamiizi wa usafiri wa majini, RVF, tayari limeonya kuhusu hatari hiyo na kueleza kuwa baadhi ya wakaazi wa Ndano na Petro Kongo hapa Kinshasa tayari wanakumbwa na hali hiyo.
Katika ripoti iliyotolewa jana Alhamisi,shirika la RVF linaomba mamlakapamoja na raia kufanya kila liwezekanalo ili kujihami dhidi ya mafuriko hayo pamoja na matokeo yake yakiwemo maradhi yanayotokana na uchafu pamoja na watu kufariki.
Swali hilo pamoja na lile la maafa mengine yaliyojiri hivi karibuni katika baadhi ya mikoa yaligusiwa jana wakati wa mkutano wa baadhi ya mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Jean-Michel Sama Lukonde. Mawaziri wanaohusika na kadhia hiyo waliamriwa kuchukuwa hatua za haraka ili kuwahudumia waathirika.
Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya, amesema waziri wa mshikamano wa kitaifa na mambo ya kibinadamu alieleza hali jinsi ilivyo pamoja na hatua zinazohitajika kuchukuliwa.
Aliongeza kuwa kwa upande wake waziri wa miundombinu alifafanua kuhusu suluhisho katika kadhia hiyo ambayo imeathiri watu kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
"Waziri mkuu aliamuru waziri wa fedha kuchukuwa hatua haraka ili kurahisisha suluhisho kwa maswala hayo yote." Alisema Muyaya katika taarifa yake.
Hali katika eneo la Kasai ni tete
Wakati wakaazi wa Kinshasa wakiarifiwa kuhusu hatari hiyo ya mafuriko pamoja na matokeo yake, familia kadhaa zimebaki bila makao huko Kananga, mji mkuu wa mkoa wa Kasaï Central baada ya mmomonyoko wa ardhi uliojitokeza mwanzoni mwa wiki.
Serikali tayari imeunda tume ili kutambua na kuorodhesha waathirikawa mkasa huo ambao umegharimu maisha ya watu kadhaa na wengine kukosa makaazi.
Mira Mulumba, mwenyekiti wa shirika la wahasiriwa wa Kongo amewasihi wakaazi waliokumbwa na mkasa huo kuwa nasubira katika wakati huu mgumu na wakati ambao serikali inaendelea kuchukua hatua.
"Naomba muwe na subra kazi itaanza hivi karibuni, kutambua na kuorodhesha wote wanaokumbwa na maafa hayo na kuwahudumia." Alisema mwenyekiti huyo.
Soma pia:'Msalaba Mwekundu' yaacha kutafuta wahanga wa mafuriko DRC
Watu wanne walifariki mwanzoni mwa wiki katika eneo la Mwenga mkoani Kivu Kusini baada ya mto mmoja kujaa na hivyo kusababisha mmomonyoko wa ardhi ukibomowa na kutupa majini nyumba zilizokuwepo.
Mkoani Mongala mafuriko yameripotiwa katika eneo la Bumba, wakati wakaazi wa eneo la Djugu mkoani Ituri nao wanakumbwa na mafuriko kufuatana na maji kutoka Ziwa Albert.