'Msalaba Mwekundu' yaacha kutafuta wahanga wa mafuriko DRC
24 Mei 2023Shirika la Msalaba Mwekundu la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limesitisha shughuli ya kuwatafuta mamia ya wahanga wa mafuriko ya hivi karibuni mashariki mwa nchi hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na kukosekana kwa mashine zinazohitajika kuchimba tope na vifusi.
Wafanyakazi wa shirika hilo wamekuwa wakiitafuta miili tangu mwanzoni mwa mwezi Mei, baada ya vijiji vya Bushushu na Nyamukubi katika jimbo la Kivu Kusini kuharibiwa na mafuriko yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 460.
Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kivu Kusini, Desire Yuma Machumu amesema kiasi cha uchafu hakiwaruhusu kuendelea kufanya kazi kwa kutumia mikono.
Amesema shughuli ya kuwatafuta wahanga inaweza ikaaza tena iwapo maafisa wa jimbo watafanikiwa kuwapatia mashine zinazotumika kuchimba.
Gavana wa Kivu Kusini, Theo Ngwabidje Kasi, amesema barabara kuelekea kwenye vijiji bado zimeharibiwa, lakini zitafunguliwa tena hivi karibuni.