Takriban watu 40 wamekufa kutokana na mafuriko nchini Kongo
28 Desemba 2023Mkazi mmoja wa Bukavu Yvonne Mukupi aliyenusurika mafuriko hayo, amesema jirani yake mmoja alisombwa na maji ya mafuriko. "Tumefanikiwa kupata miili mitatu chini ya miti lakini miili mingine bado haijapatikana, '' ameeleza Mukupi.
Vifo vyaripotiwa katika sehemu mbali mbali za Kongo
Takriban watu 20 walikufa katika eneo la Bukavu huku wengine takriban 20 wakipoteza maisha katika kijiji cha Burinyi, kilichoko umbali wa kilomita 50 kutoka Bukavu. Haya ni kwa mujibu wa maafisa katika maeneo hayo mawili.
Umoja wa Mataifa wasema mipangilio duni ya miundombinu inachangia kutokea kwa majanga
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa mipangilio duni ya miji na miundombinu dhaifu huzifanya baadhi ya jamii kuwa katika hatari zaidi ya kuathirika kutokana na mvua kubwa inayozidi kuongezeka na kunyesha mara kwa mara barani Afrika kutokana na ongezeko la joto.
"Wakati kunaponyesha , njia kuu ya maji huziba wakati mwingine kwasababu ya taka na kusababisha mafuriko yanayoharibu nyumba,'' ameeleza afisa mmoja wa Bukavu Emmanuel Majivuno aliyekuwa katika eneo hilo la tukio wakati wakazi walipokuwa wakishughulika kuokoa mali yao kutoka kwa nyumba zilizoporomoka.
Tukio hilo linafuatia vifo vya takriban watu 22 katika jimbo la Kasai-Central siku ya Jumanne wakati maporomoko ya ardhi yalipofunika nyumba, makanisa na barabara, na kuua familia nzima huku baadhi ya watu wakiachwa bila makazi.