1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouawa na mafuriko DRC yapita watu 400

Daniel Gakuba
8 Mei 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaomboleza leo mamia ya watu waliokufa katika mafuriko kwenye wilaya ya Kalehe jimboni Kivu Kusini.

https://p.dw.com/p/4R256
Demokratische Republik Kongo Überschwemmungen
Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Mkuu wa wilaya hiyo, Thomas Bakenge amesema Jumatatu kuwa idadi ya waliokufa imefika 401, na ilitarajiwa kuongezeka kwa sababu shughuli ya kuwatafuta wahanga ilikuwa ikiendelea.

Kulingana na duru kutoka eneo hilo, miili ipatayo 300 ya wahanga hao ilizikwa siku ya Jumapili.

Mvua kubwa ilianza kunyesha wilayani Kalehe jioni ya Alhamisi iliyopita, ikaifanya mito kuvunja kingo zake na kuzisomba nyumba nyingi katika vijiji vya Bushushu na Nyamukubi, na kusababisha hasara kubwa ya maisha na mali.

Afisa wa asasi ya kiraia katika eneo hilo, Delphin Birimbi amesema uharibifu wa miundombnu uliotokana na mafuriko hayo unakwamisha operesheni za uokozi.