Kongamano la ulinzi wa mazingira COP16 laanza Colombia
22 Oktoba 2024Takriban wajumbe 23,000, ikiwa ni pamoja na mawaziri 100 wa serikali na wakuu wa nchi kadhaa, waliidhinishwa kuhudhuria kongamano hilo kubwa zaidi la bioanuwai litakaloendelea hadi Novemba 1.
COP16 inajukumu la kutafuta njia za kufanikisha mafikiano ya COP15
Likiwa na kaulimbiu ya "Amani na mazingira," kongamano hilo lina jukumu la dharura la kutafuta mbinu za ufuatiliaji na ufadhili ili kuhakikisha malengo 23 ya Umoja wa Mataifa yaliyokubaliwa katika kongamano la COP15miaka miwili iliyopita yanafikiwa ifikapo mwaka 2030 ili kusitisha na kurekebisha kupotea kwa mazingira asili.
Kongamano lafunguliwa chini ya ulinzi mkali
Kongamano hilo lilifunguliwa chini ya ulinzi wa polisi na wanajeshi zaidi ya 10,000 wa Colombia baada ya kundi la wapiganaji wa EMC walio katika vita na serikali kuwaambia wajumbe wa kigeni kutohudhuria na kuonya kutofanyika kwa mkutano huo.
Wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, waakilishi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wa mataifa waliwahimiza washiriki wa kongamano hilo kutoka takriban nchi 200 kuchukuwa hatua za haraka kuchangisha mabilioni ya dola kukomesha uharibifu wa mazingira asili .
Huku takriban viumbe milioni moja vinavyojulikana kote duniani vikikadiriwa kukabiliwa na hatari ya kuangamizwa, waziri wa mazingira wa Colombia ambaye pia ni rais wa COP16 Susana Muhamad aliwaonya wajumbe hao kwamba sayari ya dunia haina muda wa kupoteza.
Yalioafikiwa katika kongamano la COP15
Miaka miwili iliyopita, nchi zilipitisha mkataba wa kihistoria wa Mfumo wa Dunia waBioanuwaiwa Kunming-Montreal na orodha ya malengo 23 ya kusaidia kukomesha kupotea kwa mazingira asili kufikia mwaka 2030. COP16 imepewa jukumu la kutafakari jinsi ya kutekeleza makubaliano hayo, yaliojumuisha kutafuta dola bilioni 200 kwa mwaka za uhifadhi.
Ulimwengu umepoteza mwelekeo kutimiza malengo ya 2030.
Siku ya Jumapili usiku, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliwatahadharisha wajumbe hao wa COP16 katika ujumbe kupitia video kwamba ulimwengu umepoteza mwelekeo katika kutimiza malengo ya 2030. Alisema wajumbe lazima waondoke kwenye mkutano huo na uwekezaji mkubwa mpya .
Mjumbe mkuu wa Brazil Andre Correa do Lago, aliliambia kongamano hilo kwamba ukosefu wa ufadhili kwa mfuko ulioko, kunaibua wasiwasi kwamba hautaweza kufikia malengo ya mfumo huo uliopitishwa.