1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kupambana na upotezaji wa bioanuwai yaanza China

Admin.WagnerD11 Oktoba 2021

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kuandaa muongozo wa kulinda na kurejesha haiba ya mifumo ya ikolojia iliyoathirika umeanza Jumatatu China.

https://p.dw.com/p/41X7W
Symbolbild Artensterben Korallen
Picha: Getty Images/D. Miralle

Mkutano huo wa siku tano wa (COP 15) unafanyika rasmi nchini China katika mji wa Kunming, lakini mengi yatafanyika mtandaoni kutokana na vikwazo vinavyotokana na janga la virusi vya corona.

Wadau wapatao 200 wanakutana, kwa lengo la kufikia makubaliano sawa na ya mkutano wa Paris wa mwaka 2015 ya kupunguza ongezeko la joto duniani.

Akiwa katika ufunguzi wa mkutano huo, makamu wa Waziri Mkuu Han Zheng, amesema China itajumuisha ulinzi wa bioanuai katika mipango yake ya maendeleo ya mikoa na sekta zote, na kuandaa mkakati wa kitaifa wa hifadhi.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa kwanza kuhusu mzozo wa Bioanuwai

Kamati ya Bioanuwai ya Chuo cha Sayansi cha China (CAS) ilitangaza Jumapili mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuhifadhi bioanuwai, hasa matumizi ya satelaiti na teknolojia nyingine kwenye miaka ya hivi karibuni.

"China imeonyesha mwelekeo wa kuongoza ulimwenguni kote kwenye suala la utafiti wa kuhifadhi bioanuwai, hasa utumiaji wa teknolojia, China pia inaongoza mstari wa mbele katika utafiti wa kuchunguza asili, mabadiliko ya bioanuwai, na pia katika utafiti wa wanyama walio hatarini kutoweka na jinsi ya kuwalinda," ameeleza Wei Fuwen mwanachama wa kamati ya (CAS).

Albanien Forscher kämpfen gegen Verschwinden der adriatischen Meereswälder
Picha: GENT SHKULLAKU/AFP

Wasiwasi kuhusu China

Wataalam hata hivyo wana wasiwasi juu ya athari za kimazingira kote ulimwenguni, zinazotokana na maendeleo ya kiuchumi ya China.

Nathalie Seddon, Profesa wa Bioanuwai katika Chuo Kikuu cha Oxford anaonya kuwa ulimwengu lazima uhakikishe ahadi hizo za China zinatekelezwa kimataifa. Kwani China inaweza kuchukua hatua za kulinda mifumo ya ikolojia ya ndani ya nchi yake, lakini biashara zake zinaathiri zaidi viumbe hai vya nje ya nchi, kama vile barani Afrika na Amerika ya Kusini.

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa unaohusu viumbe hai sio maarufu kama ulivyo mkutano ujao wa umoja huo huo unaohusu Mabadiliko ya Tabianchi, ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi huu nchini Scotland.

Soma zaidi: WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani

Mkuu wa mkutano huo wa viumbe hai wa Umoja wa Mataifa Elizabeth Maruma Mrema amesema wakati wa ufunguzi hii leo, kwamba ulimwengu haukuweza kupata mafanikio yaliyotarajiwa kutoka mwaka 2011 hadi 2020, na pia umeshindwa kuilinda mifumo ya ikolojia ambayo ni muhimu kwa ustawi wa binadamu.

Duru ya kwanza ya mazungumzo ya "COP15" kuhusu bioanuwai ya ulimwengu inaaanza leo Oktoba 11 na kumalizika Oktoba 15. Na mkataba wa maafikiano wa kulinda bioanuwai ya ulimwengu unatarajiwa kukamilika wakati wa duru ya pili ya mkutano huo mwakani mnamo miezi ya Aprili-Mei.

Vyanzo (dpa,rtre)