Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer yuko ziarani Berlin
28 Agosti 2024Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer yuko mjini Berlin ambako atakuwa na mazungumzo na viongozi wa Ujerumani kujadili makubaliano ya kihistoria ya kiuchumi na ulinzi.
Kiongozi huyo anatarajia kutumia ziara yake hiyo ya siku mbili Ujerumani na Ufaransa kurekebisha mahusiano na Umoja wa Ulaya.
Dhamira ya waziri mkuu wa Uingereza ni kurekebisha mahusiano
Waziri mkuu Keir Starmer anataka kuiona Uingereza inarekebisha mahusiano na washirika wake Umoja wa Ulaya, na kujiondowa katika mwelekeo uliochukuliwa huko nyuma na serikali zilizoongozwa wa wahafidhina, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uchumi wa taifa hilo.
Ziara yake katika kanda ya Umoja wa Ulaya imeanzia hapa Ujerumani mjini Berlin alikowasili jana Jumanne, na leo Jumatano amekwisha kutana na rais Frank Walter Steinmeier baada ya kulitembelea eneo maarufu la lango la kihistoria la Brandenburg.
Na baadae akakaribishwa kwa heshima za kijeshi na Kansela Olaf Scholz kwenye ofisi ya Kansela.
Viongozi hao watajadili mkataba mpya ambayo wote wanataraji utaleta ushirikiano wa kijeshi na kuimarisha zaidi ushirikiano katika maeneo kadhaa ikiwemo biashara na nishati. Baadae mchana watafanya mkutano na waandishi habari.
Anachokisisitiza waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer kwenye ziara hii ni hasa kuyabadilisha mahusiano kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya ambayo yamepwaya tangu nchi hiyo ilipoamuwa kujiondowa katika Umoja huo.Soma pia: Umoja wa Ulaya waionya Uingereza kuhusu mktaba wa Brexit
Hata taarifa yake aliyoitowa inaonesha hivyo. Starmer amesema wanabidi Uingereza hivi sasa kutumia fursa hii ya kipekee kuyarekebisha mahusiano na Umoja wa Ulaya.
Wasiwasi wa washirika kuhusu Trump
Uingereza na Ujerumani,ambazo ni washirika wa jumuiya ya kijeshi ya NATO na wenye bajeti kubwa za kijeshi katika kanda ya Ulaya Magharibi,hivi sasa wanatafuta njia ya kuimarisha mahusiano ya kijeshi kabla ya uwezekano wa Marekani kuchukuwa hatua ya kupunguza msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine,ikiwa Donald Trump atarejea madarakani mwanzoni mwa mwaka ujao.Starmer afanya ziara Berlin kujadili mkataba na Ujerumani
Yote haya ni kwasababu tayari mgombea huyo wa uchaguzi wa rais nchini Marekani kutoka chama cha Republican ameshatahadharisha kwamba ikiwa ataingia Ikulu,kwahakika kabisa,atatafakari umuhimu,au malengo ya taasisi ya NATO na shughuli zake.
Trump pia alishasema waziwazi kwamba hatokuwa tayari kupeleka msaada mwengine zaidi kwa Ukraine na pia hatowatetea ncvhi washirika ambao hawatokuwa tayari kuongeza bajeti zao za ulinzi.
Malengo ya Berlin na London ni yapi?
Kwahivyo Berlin na London zinataka kuanzisha ushirikiano wa kiulinzi na huenda ukafanana na ule uliofikiwa kati ya Uingereza na Ufaransa mnamo mwaka 2010 kwa mujibu wa maafisa, huku zikitoka ahadi za kuundwa kikosi cha pamoja na kushirikiana katika suala la kubadilishana vifaa na matumizi ya vituo vya kuendesha utafiti wa silaha za makombora ya Nyuklia.Soma pia: Mfalme Charles III wa Uingereza kufanya ziara nchini Ujerumani
Waziri mkuu wa Uingereza pia atafanya mazungumzo nchini Ujerumani na wakuu wa makampuni ikiwemo mkurugenzi mkuu mtendaji wa kampuni kubwa la utengenezaji silaha la Rheinmetall,Armin Papperger ambaye vyomvo vya habari mwezi uliopita viliripoti kwamba alilengwa na Urusi katika njama ya kuuliwa,japo Urusi ilisema zilikuwa taarifa za uwongo.
Baada ya mazungumzo yake mjini Berlin ataelekea Paris kushiriki sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya walemavu itakayoanza usiku na atakutana na wakuu wa makampuni mbali mbali kesho Alhamisi.