Mfalme Charles III wa Uingereza kufanya ziara Ujerumani
28 Machi 2023Mfalme Charles atawasili mjini Berlin na kuhudhuria shughuli mbalimbali huko Brandenburg kabla ya kuelekea Hamburg katika ziara yake ya siku tatu.
Uamuzi wa kuwatembelea kwanza majirani wa karibu unachukuliwa kama jaribio la kufufua uhusiano baada ya Uingereza kujiondoa katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, kitendo kinachofahamika zaidi kama "Brexit".
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema hatua hiyo ni ishara muhimu kwa Ulaya, na kuongeza kuwa ziara hii inadhihirisha urafiki wa karibu na wa dhati kati ya nchi hizo mbili.
Rais Steinmeier na mkewe Elke Buedenbender watawakaribisha Mfalme Charles na Malkia Camilla kwa heshima na kwa kuzingatia itifaki za kijeshi huko Brandenburg. Baadaye, Mfalme na Malkia watasafiri hadi kwenye Kasri la Steinmeier la Bellevue katikati mwa jiji la Berlin, ambako itaandaliwa karamu ya kitaifa kwa ajili ya familia hiyo ya kifalme.
Siku ya Alhamisi Mfalme Charles atatoa hotuba katika bunge la shirikisho la Ujerumani na kukutana na wakimbizi waliowasili hivi karibuni kutoka nchini Ukraine. Baadaye viongozi hao watatembelea kituo cha kijeshi cha Ujerumani na Uingereza kilichopo katika jimbo la Brandenburg.
Siku ya Ijumaa, Mfalme Charles ataelekea katika mji wa bandari wa kaskazini wa Hamburg ambako anatarajiwa kuzuru mradi wa nishati mbadala isiyo chafuzi kwa mazingira.
Bob Ward, kutoka chuo cha Uchumi cha London amesema haishangazi kwamba baada ya kuwa mfalme hajaachana na mapambano yake ya muda mrefu katika masuala ya mazingira.
Ward ameongeza kuwa hili ni suala linalovuka mipaka ya kisiasa na kwamba Mfalme Charles kama mkuu wa nchi, hawezi kukosa kuzungumzia suala muhimu kama hilo.
Soma pia: Mfalme Charles kuanza ziara Ujerumani
Mfalme Charles wa Uingereza na Rais Steinmeier wa Ujerumani wataweka mashada ya maua katika magofu ya kanisa la Mtakatifu Nikolai mjini Hamburg, ambalo liliharibiwa wakati wa uvamizi wa anga wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na ambalo kwa sasa linatumika kama eneo la makumbusho.
Mfalme huyo wa Uingereza atasaini pia kile kinachoitwa "Kitabu cha Dhahabu" cha jiji hilo la Hamburg, ambacho aliwahi kukisaini hapo awali mnamo mwaka 1987 wakati wa ziara yake akiwa na mkewe wa wakati huo Princess Diana.
Mfalme Charles III adhamiria ziara yake
Rais Ujerumani amesema alitoa mwaliko huo kwa Charles, ambaye ametembelea Ujerumani kwa zaidi ya mara 40, wakati wa mazishi ya mama yake, Malkia Elizabeth II, mwezi Septemba mwaka jana.
Steinmeier amesema kuona Mfalme Charles anaizuru Ujerumani karibu miezi sita baadaye, inaonyesha ni jinsi gani mfalme huyo anathamini urafiki kati ya mataifa hayo na kwamba wote wanataka uhusiano wa karibu na wa kirafiki hata baada ya Brexit.
Mfalme Charles ameonyesha nia madhubuti ya kuanza ziara yake hiyo ya kwanza ya kiserikali akiwa kama mfalme, baada ya safari yake nchini Ufaransa, ambayo ilikusudiwa kufanyika mapema wiki hii, kuahirishwa kutokana na maandamano ya vurugu kufuatia mpango wa marekebisho ya pensheni.
Soma pia: Mfalme Charles kuzuru Ujerumani na Ufaransa
Ziara hiyo ilikusudia kuangazia hali ya uhusiano kati ya Ufaransa na Uingereza, lakini badala yake itaangazia maandamano makubwa yanayoikumba Ufaransa miezi 10 tu katika muhula wa pili wa Rais Emmanuel Macron.
Macron aliwaambia waandishi wa habari kwamba majadiliano juu ya kupanga upya ziara hiyo ya Mfalme Charles yanaweza kufanyika katika miezi ijayo, na kwamba wamependekeza ziara hiyo ifanyike mwanzoni mwa msimu ujao wa joto.