1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatanua mashambulizi Rafah, mzozo ukizidi na Mareani

21 Juni 2024

Vikosi vya Israel vimeushambulia mji wa Rafah na maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza na kupambana na wapiganaji wa Hamas, katika hatua iliyoelezwa kuwa jaribio la jeshi la Israel kukamilisha utekaji wao wa mji wa Rafah.

https://p.dw.com/p/4hLxk
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant akizuru vikosi vya makombora vinavoytoa msaada kwa wanajeshi wa IDF katika operesheni ya eneo la Rafah.Picha: Ariel Hermoni/Israel Mod/IMAGO

Vifaru vya Israel vimeonekana vikielekea magharibi na kaskazini mwa mji wa Rafah; baada ya kuyateka maeneo ya mashariki, kusini na katikati, huku vikosi vyake vikishambulia kutokea kwenye ndege, vifaru na meli nje ya pwani ya Gaza, na kusababisha wimbi jipya la wakimbizi kutoka mji huo, ambao ulikuwa unahifadhi zaidi ya watu milioni moja waliopoteza makazi yao, na wengi wao wakilaazimika kuhama tena.

"Nimehamishwa karibu mara tano. Nilihamishwa kwa mara ya kwanza hadi eneo la Nusseirat. Baada ya hapo, nilihama kutoka Nusseirat hadi Khan Yunis na kutoka Khan Younis nilihamishwa hadi Rafah. Na sasa nimehama kutoka Rafah hadi Khan Younis kwa sababu ya makombora yaliyotuzunguka na hofu. Kwa sasa niko katika eneo la Khan Younis. Kama unavyoona, mahali hapa ni jangwa na hakuna maji au mambo yoyote ya maisha," alisema Muhammad Hani".

Ukanda wa Gaza| Vita vya Israel-Hamas
Mashambulizi ya Israel yamekuwa yakiwahamisha wakaazi wa Gaza kutoka eneo moja kwenda jengine kwa kipindi chote cha vita vya Gaza.Picha: Doaa Albaz/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israel lilisema Ijumaa kuwa vikosi vyake vilikuwa vikifanya mashambulizi ya usahihi kwa kutumia taarifa za ujasusi katika eneo la Rafah, ambapo wanajeshi wake wameshiriki mapambano ya mtaani na na walikuwa wamegundua njia za chini kwa chini zinazotumiwa na wanamgambo.

Soma pia: Msemaji wa jeshi la Israel asema Hamas haiwezi kusambaratishwa

Kikosi cha Al-Qassam ambacho ni tawi la kijeshi la Hamas kilisema siku ya Alhamisi kuwa wapiganaji wake walipiga vifaru viwili vya Israel kwa roketi za kushambulia vifaru katika kambi ya Shaboura mjini Rafah, na kuwaua wanajeshi waliojaribu kukimbia kupitia vichochoro. Hata hivyo hakukuwa na tamko la mara moja kutoka Israeli juu ya madai ya Hamas.

Mzozo mpya kati ya White House na Netanyahu

Hayo yanajiri wakati mzozo mpya ukijitokeza kati ya Israel na mfadhili wake mkuu Marekani, kuhusiana na madai ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kwamba utawala wa Rais Joe Biden uliizuwilia Israel silaha na risasi kwa miezi kadhaa, madai ambayo Ikulu ya Marekani iliataja kuwa "ya kuhuzunisha" na "ya kukatisha tamaa".

Rais Joe Biden na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kulia, ameituhumu utawala wa Rais Joe Biden, kushoto, kwa kuizuwilia Israel silaha katika miezi kadhaa iliyopita.Picha: Miriam Alster/UPI Photo/imago images

''Hakika inakatisha tamaa, hasa ikizingatiwa kwamba hakuna nchi nyingine inayofanya zaidi kuisaidia Israel kujilinda dhidi ya kitisho cha Hamas na vitisho vingine vinavyowakabili katika eneo hilo kama Marekani. Namaanisha, Mungu wangu, rais huyu aliweka ndege za kivita za Marekani angani katikati ya mwezi wa Aprili ili kusaidia kudungua mamia ya droni na makombora, yakiwemo ya masafa marefu yaliyorushwa na Iran dhidi ya Israel,'' alisema John Kirby, Msemaji wa Baraza la Taifa la Usalama la White House.

Soma pia: Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha

Suala hilo lilianza wakati Netanyahu alipodai katika video iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii mapema wiki hii kwamba utawala wa Marekani -- mfadhili mkuu wa kijeshi wa Israel -- umekuwa "ukiinyima nchi yake silaha na risasi" katika miezi ya hivi karibuni.

Lakini Netanyahu alionekana kusisitiza msimamo wake siku ya Alhamisi, akisema katika taarifa kwamba "yuko tayari kukabiliwa na mashambulizi ya kibinafsi al-mradi Israel itapokea zana inazozihitaji kutoka kwa ajili ya uwepo wake.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewaambia maafisa wa Israel wakati wa mkutano jana Alhamisi, kwamba wanapaswa kuepusha kuchochea mzozo wa Lebanon wakati vita vya Gaza vikiendelea. Blinken alikutana na mshauri wa usalama wa taifa wa Israel Tzachi Hanegbi na Ron Dermer, waziri wa masuala ya kimkakati wa Israel.

Armenia yaitambua Palestina kama taifa huru

Armenia imeungana na orodha ya mataifa kadhaa yaliotangaza kulitambua taifa la Palestina katikati mwa vita vya Gaza, ikisema inapinga vurugu dhidi ya raia.

Mataifa kadhaa yamelitambua Taifa la Palestina katikati mwa vita kati ya Israel na Hamas, na kukemewa vikali na maafisa wa Israel.x

Soma pia: Uhispania, Ireland na Norway zaitambua rasmi Palestina

"Katika kuthibitisha dhamiri yake kwa sheria za kimataifa, usawa wa mataifa, mamlaka na kuishi pamoja kwa amani, Jamhuri ya Armenia inatambua Taifa la Palestina," Yerevan ilisema.

Armenia iliongeza kuwa "ina nia ya dhati ya kujenga amani ya muda mrefu na utulivu katika Mashariki ya Kati."

Yerevan, ambayo yenyewe imekumbwa na mzozo na nchi jirani ya Azerbaijan kwa miongo kadhaa, ilikosoa vikali mwenendo wa kijeshi wa Israel huko Gaza.

Chanzo: Mashirika