1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya anga ya Israel yauwa watu 35 Ukanda wa Gaza

23 Mei 2024

Duru za ndani nchini Israel zinasema serikali ya taifa hilo itatoa karipio kali (23.05.2024) kwa mabalozi wa Ireland, Norway na Uhispania kutokana na mpango wa serikali zao wa kulitambua taifa la Palestina juma lijalo.

https://p.dw.com/p/4gC3I
Gaza | Rafa | Jengo la makazi lililoharibiwa na shambulio la anga la Israel
Mpalestina na watoto wake wameketi katika chumba kilichoharibiwa kufuatia shambulio la anga la Israel huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza Mei 22, 2024.Picha: Eyad Al-Baba/AFP/Getty Images

Taarifa hiyo inatolewa wakati ndani ya Ukanda wa Gaza Wapalestina 35 wakiripotiwa kuuwawa kwa mashambulizi ya jeshi lake usiku wa kuamkia leo (23.05.2024).

Mabalozi hao wameitwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ambapo pamoja na masuala mengine wataoneshwa vidio ambazo hazijaoneshwa hadharani za Hamas wakiwachukua mateka wanawake wakati wa shambulio la Oktoba 7 kwa Israeli ambalo lilizusha vita vya Gaza. Israel pia imewaita tena mabalozi wake huko Dublin, Oslo na Madrid kwa mashauriano.

Akizungumzia suala la utambuzi wa taifa la Palestina Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia, Luis Gilberto Murillo alisema, "Kwa hivyo tunaamini, tuna uhakika kwamba nchi nyingi zaidi zitaitambua Palestina na hii sio dhidi ya Israeli au watu wa Israeli au Wayahudi. Umoja wa Mataifa uliridhia, katika muktadha wa Makubaliano ya Oslo, kwamba suluhisho la serikali mbili linapaswa kuundwa na hivyo kama unahitaji mataifa mawili basi ni wazi kwamba hilo linahitaji Palestina kutambuliwa kama taifa."

ICJ kutoa uamuzi wa kusitisha vita Gaza

Gaza | Deir al-Balah | Al-Zawaida | Majengo yaliyoharibiwa na shambulizi la anga la Israel
Wapalestina wakikagua uharibifu kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel mapema Mei 22, 2024Picha: Bashar Taleb /AFP/Getty Images

Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa (ICJ) imesema leo hii inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi la Afrika Kusini la kuitaka Israel kutekeleza usitishaji vita huko Gaza. Afrika Kusini imeiomba Mahakama ya Kimataifa kuchukua hatua za dharura kuiamuru Israel "kusitisha operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza" ikiwa ni pamoja na katika mji wa Rafah, ambako inashinikiza kufanya mashambulizi.

Maamuzi ya ICJ, ambayo ina nguvu ya kutoa uamuzi kuhusu mizozo kati ya mataifa, ina wajibu huo lakini haina mamlaka ya kufanikisha utekelezaji. Na itakumbukwa katika vita vya Urusi na Ukraine ilitoa uamuzi wa Urusi kusitisha uvamizi wake kwa Ukraine bila mafanikio yoyote.

Lakini uamuzi dhidi ya Israel utaongeza shinikizo la kisheria la kimataifa baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kusema Jumatatu kuwa yupo katika juhudi ya kufanikisha utowaji wa waranti za kukamatwa kwa viongozi wakuu wa Israel na Hamas.

Watu 35 wameuwawa katika mashambulizi Gaza

Wakati hayo yakijitokeza vifaru vya Israel leo pia vimeonekana kusonga mbele katika maeneo ya pembezoni mwa wilaya hiyo yenye idadi kubwa ya watu ya Rafah  matukio yanayeondelea ikiwa ni siku ya kuamkia usiku wa kuamkia leo ambao ulikuwa na mashambulizi zaidi huko katika maeneo ya kusini mwa Gaza tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake katika maeneo hayo mapema mwezi huu.

Israel inasema haina budi ila kuushambulia mji huo kwa lengo la kile wanachosema kuwamaliza kabisa wapiganaji wa Hamas ambao inaamini ni wamejificha huko. Wanajeshi wake wamekuwa wakiingia polepole ndani viunga vya mashariki mwa Rafah tangu mwanzoni wa mwezi. Ambapo kwa usiku wa kuamkia leo Wapalestina 35 wameripotiwa kuuwawa kufuatia mashambulizi ya angani ya jeshi la Israel.

Soma zaidi:Norway, Ireland, Uhispania kutambua taifa la Palestina

Wakati jeshi la Israel likiendelea na operesheni zake, bado inasema iko tayari kuanzisha tena mazungumzo yaliyokwama juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka na Hamas ili kusitisha vita vinavyoendelea tangu Oktoba 7. Shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano limeongezeka kwa Israel na Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu huku nchi tatu za Ulaya Jumatano ziliweka wazi kuwa zitalitambua taifa la Palestina.

Vyanzo: RTR/AFP