Blinken: Nchi za kiarabu ziishinikize Hamas kukubali suluhu
10 Juni 2024Alipotua mjini Cairo kabla ya kuelekea Israel, Blinken amewaambia waandishi wa habari kuwa viongozi na watu wa Mashariki ya Kati wanapaswa kuishinikiza Hamas kukubaliana na pendekezo la upatanishi la Marekani katika mzozo huu unaoendelea huko Gaza.
"Ujumbe wangu kwa serikali na watu katika eneo hili ni kwamba, kama mnataka kusitishwa kwa mapigano, muishinikize Hamas ikubali. Ikiwa mnataka kupunguza mateso ya Wapalestina huko Gaza, kuwarejesha mateka wote nyumbani, kuwaweka Waisraeli na Wapalestina kwenye njia ya amani na usalama wa kudumu na kama mnataka kuzuia mzozo huu usitanuke, basi muishinikize Hamas kuafiki mpango huu wa usitishwaji mapigano."
Aidha Blinken amesema anaamini kuwa idadi kubwa ya watu ima wawe Israel, Ukingo wa Magharibi au hata Gaza, basi matumaini yao ni kuona katika siku zijazo Waisraeli na Wapalestina wanaishi kwa amani na usalama.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani ameishutumu Hamas na kusema ni wao pekee ambao hadi sasa hawajaafiki pendekezo hilo la awamu tatu linaohusisha kusitisha mapigano, kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina pamoja na kuanzisha mazungumzo ya kujadili kuhusu ujenzi wa Gaza baada ya vita.
Soma pia: Israel yashambulia kambi wakati vita vya Gaza vikiingia mwezi wa tisa
Afisa mwandamizi wa Hamas Abu Zuhri ameikosoa kauli ya Blinken na kusema ni yenye "upendeleo" kwa Israel na kwamba msimamo huo ni kikwazo cha kufikiwa makubaliano, na kwamba hii inadhihirisha kuwa Marekani inaafiki mauaji ya kimbari
yanaofanywa na wavamizi wa Gaza.
Blinken akutana na rais al-Sisi mjini Cairo
Antony Blinken ambaye baadaye wiki hii ataelekea pia Jordan na Qatar, amekutana na kuzungumza na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kuhusu vita hivi vya umwagaji damu huko Gaza ambavyo hadi sasa vimekwisha sababisha vifo vya watu 36,730 hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas. Viongozi hao wawili wameahidi kuungana ili kufanikisha mpango huo wa usitishwaji mapigano.
Soma pia: Hamas yaitaka Marekani kuishinikiza Israel kusitisha vita Gaza
Huko Gaza kwenyewe vita vinaendelea huku hali jumla ya kibinaadamu ikizidi kuwa mbaya. Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameeleza kuwa ifikapo katikati mwa mwezi Julai mwaka huu, zaidi ya watu milioni moja huko Gaza wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya njaa. Wapalestina wanakabiliwa pia na uhaba wa bidhaa muhimu kama vile dawa, maji na vifaa vingine.
(Vyanzo: Mashirika)