Israel yalaumiwa katika ripoti mpya ya Amnesty International
5 Desemba 2024Ripoti hiyo ya Shirika la Amnesty International imeishutumu Israel kwa "kufanya mauaji ya halaiki" dhidi ya Wapalestina huko Gaza tangu kuanza kwa vita mwaka jana. Amnesty International imesema ripoti yake hiyo mpya inalenga kupaza sauti kwa jumuiya ya kimataifa.
Soma Pia: Umoja wa Mataifa wasema machafuko yameongezeka Gaza
Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London, Uingereza lisema matokeo ya ripoti yake yametokana na matamko ya kuudhalilisha utu yanayotolewa na maafisa wa serikali ya Israel pamoja na mauaji ya halaiki yaliyoorodheshwa kutoka kwenye picha za satelaiti zinazoonesha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza na pia ripoti zilizokusanywa moja kwa moja kutoka kwa watu wa Gaza.
Katibu Mkuu wa Shirika la Amnesty International, Agnes Callamard, amesema kwenye ripoti hiyo mpya kuwa mwezi baada ya mwezi, Israel imeendela kuwageuza Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kuwa kama kikundi cha watu wasiostahili haki za binadamu wala utu.
Kwa upande wake Israel imepinga vikali shutuma hizo, ikisema vitendo vyake ni vya kujilinda na imekumbusha juu ya haki yake ya kujilinda.
Chanzo cha mzozo wa Gaza kilikuwa mashambulizi yaliyofanywa na kundi la wanamgambo wa Hamas na wapiganaji wengine wenye msimamo mkali mnamo Oktoba 7, mwaka 2023 katika eneo la Kusini mwa Israel. Watu wapatao 1,200 waliuawa na wengine wapatao 250 walichukuliwa mateka.
Soma Pia: Hamas yatishia kuwaua mateka wa Israel ikiwa Israel itafanya operesheni ya kuwaokoa mateka
Katibu Mkuu wa Shirika la Amnesty International Agnes Callamard, amesema ripoti hiyo mpya ya kusikitisha lazima ichukuliwe kama wito wa kuiamsha jumuiya ya kimataifa kwamba haya ni mauaji ya halaiki na kwamba kila linalowezekana lifanyike kuyakomesha haraka.
Vyanzo: AFP/DPA/AP