1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Israel ikomeshe mateso kwa Wapalestina Gaza

18 Julai 2024

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeitaka Israel kusitisha mateso kwa watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4iTos
Nembo ya Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International
Nembo ya Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International Picha: Pond5 Images/IMAGO

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Israel kuachana na vitendo vya kuwaweka gerezani Wapalestina kwa muda usiojulikana na bila kufunguliwa mashtaka.

Amnesty imeongeza kuwa mamlaka za Israel zinatakiwa kukomesha kile walichokiita "mateso yaliyokithiri" katika magereza hayo na kusisitiza kuwa vitendo vyote hivyo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Soma pia: Operesheni mpya ya Kijeshi Gaza yakosolewa na UN

Amnesty imetoa pia wito wa kufutwa kwa sheria inayowalenga "wapiganaji haramu", ambayo ilifanyiwa marekebisho tangu kuanza kwa vita vya Gaza, sheria ambayo inaruhusu majeshi ya Israel kuwashikilia watu kwa miezi kadhaa bila ya kuwafungulia mashtaka au kuhukumiwa. Shirika hilo limesema sheria hiyo inawezesha mateso yaliyokithiri na kwa namna fulani imepelekea watu kutoweka katika mazingira tatanishi.

Mchakato wa mazungumzo waendelea

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akishiriki mkutano na viongozi kadhaa wa PalestinaPicha: Thaer Ganaim/apaimages/IMAGO

Ujumbe wa Israel kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano umewasili mjini Cairo nchini Misri kuendelea na mazungumzo hayo na juu ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel wakati amapo mashambulizi yakiendelea huko Gaza.

Wajumbe hao wa Israel wamewasili Misri kuendelea na mazungumzo hayo wakati Israel na Hamas  wakionesha nia ya kuzingatia pendekezo lililowasilishwa hivi karibuni. Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na maafisa watatu wa Misri, ambao hata hivyo hawakutoa maelezo zaidi.

Wapatanishi wa kimataifa wakiongozwa na Marekani, Misri na Qatar wanazishinikiza pande mbili kwenye mzozo huo kuafiki makubaliano ambayo kwa awamu yatawezesha usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka wapatao 120 ambao bado wanashikiliwa na Hamas huko Gaza.

Mazungumzo hayo yalivurugika mwishoni mwa juma baada ya Israel kufanya mashambulizi makubwa na kudai ilikuwa ikiwalenga makamanda wa jeshi la Hamas, shambulio ambalo hata hivyo lilisababisha vifo vya raia wasiopungua 90 na kuwajeruhi mamia ya wengine.

Vita vyasababisha hali mbaya ya kiutu Gaza

Raia wa Palestina wakiwatafuta manusura baada ya shambulizi huko Nuseirat, Gaza
Raia wa Palestina wakiwatafuta manusura baada ya shambulizi huko Nuseirat, GazaPicha: EYAD BABA/AFP/Getty Images

Siku ya Alhamisi pia, mashambulizi yameripotiwa katika maeneo mbalimbali kwenye ukanda wa Gaza.  Rajaa Abu Rakab, alishuhudia mwanae, mjukuu na mkwe wake wakiuawa kufuatia mashambulizi ya usiku wa kuamkia Alhamisi:

" Walimwengu wako wapi? Kila mtu anasema kuna suluhisho, lakini halipatikani. Tunakufa na tunaangamizwa, huku tukiangalia watoto wetu wakiuawa na kupokonywa kutoka mikononi mwetu, tunaamka na kulala tukiwa na hofu."

Soma pia: ICRC: Vituo vya afya vimeelemewa mno huko Gaza

Hali ya kibinaadamu ni ya kusikitisha eneo hilo ambapo Shirika la Msalaba mwekundu limeonya hivi leo kuhusu hali mbaya ya vituo vya afya ambavyo vimeelemewa kutokana na ongezeko la majeruhi. Kumekuwa pia kukiripotiwa  uhaba wa chakula, maji safi na bidhaa nyingine muhimu.

Italia imetangaza hii leo kuwa imetuma msaada wa kibinaadamu wa chakula na vifaa vya afya kwa wakazi wa Gaza kwa kutumia ndege iliyotua nchini Jordan. Msaada huo unajumuisha zaidi ya tani 60 za chakula, vifaa vya matibabu pamoja na mahema yapatayo 150.

(Vyanzo: DPAE, AP, AFP)