1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS na juhudi za kidiplomasia kwenye mzozo wa Niger

Angela Mdungu
13 Agosti 2023

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS imeendeleza juhudi zake za kutafuta njia za kidiplomasia za kubatilisha mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Niger mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/4V74M
Rais wa Nigeria na Mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS Bola Tinubu.
Rais wa Nigeria na Mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS Bola Tinubu.Picha: Gbemiga Olamikan/AP/dpa/picture alliance

Juhudi hizo zinafanyika wakati ECOWAS ikiiendeleza msimamo wake wa kutishia kuingilia kati kijeshi kwenye taifa hilo katika mzozo huo mkubwa uliozivuta nchi zenye nguvu duniani.

Jumuiya hiyo, jana Jumamosi ilisema kwamba imedhamiria kutuma kamati ya bunge ili ikutane na viongozi wa mapinduzi ambao wanamshikilia Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum, na wameshavunja serikali yake. Mapinduzi ya kijeshi ya Niger ni ya saba Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati katika kipindi cha miaka mitatu.

Soma zaidi: ECOWAS waamua kujizuia kuingilia kati kijeshi Niger

Msemaji wa bunge la ECOWAS amesema kuwa licha ya kuwa bunge hilo halikufanya maamuzi thabiti Jumamosi, liliunda kamati inayopanga kuonana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye kwa sasa anakalia uenyekiti wa kupokezana ili ipate ruhusa yake ya kwenda Niger.

Viongozi wa mapinduzi wakiongozwa na Jenerali Tiani, wamekataa juhudi za awali za kidiplomasia za ECOWAS, Marekani na nchi nyingine jambo linaloweza kuongeza mzozo katika kanda masikini ya Sahel ambayo  tayari inakabiliwa na makundi ya itikadi kali.

Ushawishi wa mataifa yenye nguvu Afrika Magharibi, Afrika ya Kati hatarini.

Kutokana na mzozo huo, si tu hatma ya Niger ambayo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya Urani na mshirika wa mataifa ya magharibi katika vita dhidi ya makundi ya itikadi kali iliyo mashakani, bali pia ushawishi wa mataifa hasimu yenye nguvu duniani ambayo yana maslahi ya kimkakati kwenye eneo la Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.

Jenerali Abdourahamane Tiani
Jenerali Abdourahamane TianiPicha: ORTN/Télé Sahel/AFP/Getty Images

Wanajeshi wa Marekani, Ufaransa na Italia wako Niger, katika ukanda ambao washirika wa ndani wa al Qaeda na kundi linalojiita dola la Kiislamu wameshawauwa maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni wayakimbie makazi yao.

Soma zaidi: Viongozi wa mapinduzi Niger wasema hawawezi kuupokea ujumbe wa ECOWAS

Ushawishi wa Urusi umekuwa ukikua wakati pia ukosefu wa usalama ukiongezeka. Demokrasia nayo imezorota na viongozi wanatafuta washirika wapya ili kurejesha utaratibu.

Mataifa ya magharibi yana wasiwasi kuwa Ushawishi wa Urusi huenda ukaongezeka kama wanajeshi waliofanya mapinduzi watafuata hatua za Mali na Burkina Faso ambazo zilvifukuza vikosi vya mtawala wao wa zamani, Ufaransa baada ya mapinduzi ya nchi hizo.