Jumuiya ya ECOWAS inaweza kuziwajibisha tawala za kijeshi?
2 Agosti 2023Hata hivyo kwa kipindi chote kilichopita tangu kuundwa kwake, vikwazo vya jumuiya hiyo dhidi ya nchi wanachama vimesadifu kutokuwa na nguvu yoyote, hali iliyofichua udhaifu wa ECOWAS.
Siku kadhaa tu baada ya mapinduzi, ECOWAS iliitumia ujumbe kwa Niger, taifa mwanachama wa jumuiya hiyo, kuwa ina wiki moja pekee ya kurejesha utawala wa kikatiba au ikabiliwe na vikwazo vikali vya kiuchumi.
Pia ECOWAS ilitahadharisha kwamba "inaweza kutumia hatua zozote zinazofaa kurejesha msingi wa kikatiba” nchini Niger, ikiwezekana hata matumizi ya nguvu.
Niger ni taifa la nne mwanachama wa ECOWAS kuanguka chini ya mikono ya wanajeshi walioiondoa serikali halali madarakani. Mataifa mengine ya Guinea, Burkina Faso na Mali nayo yalishuhudia mapinduzi ya kijeshi miaka michache iliyopita.
Msimamo wa ECOWAS kwa matendo hayo umekuwa mzito kuliko ilivyotarajiwa lakini swali linalosalia, je, jumuiya hiyo ina nguvu na uwezo wa kweli, kushughulikia kadhia ya mapinduzi ya kijeshi magharibi mwa Afrika?
ECOWAS: Jumuiya imara na muhimu ya kiuchumi
Jumuiya ya ECOWAS iliundwa mwaka 1975 nchini Nigeria kwa kutiwa saini mkataba wa Lagos ambao ulipitiwa upya kwa marekebisho machache mjini Cotonou nchini Benin mnamo 1993.
Jumuiya hiyo ina nchini wanachama 15 ambazo kwa jumla zina idadi ya watu milioni 400 na kuifanya kuwa moja ya taasisi kubwa ya kikanda barani Afrika, hususani kiuchumi.
Kwenye tovuti yake, ECOWAS inajipambanua kuwa na dira ya kuunda kanda isiyo na vizuizi vya mipaka ambayo inawapa watu wake fursa ya kufanya biashara na kushirikiana kiuchumi bila vizingiti huku wakiishi kwa misingi ya utu, amani na usalama. Msisitizo wa dira ya ECOWAS umewekwa zaidi kwenye eneo huru la kiuchumi baina ya nchi wanachama.
Mataifa nane yaliyokuwa makoloni ya Ufaransa ambayo sasa ni wanachama wa ECOWAS yanatumia sarafu moja ya Faranga CFA. Sarafu hiyo ina mafungamano makubwa na iliyokuwa sarafu ya zamani ya Ufaransa, Faranga na hivi sasa sarafu ya Euro.
Juhudi za kufikia itifaki ya kuwa na sarafu moja ndani ya ECOWAS ili kuondoa utegemezi kwa sarafu ya Euro zimekuwepo kwa muda mrefu bila mafanikio.
ECOWAS: Chombo kisicho na nguvu mbele ya ugaidi?
Kanuni zinaoongoza ECOWAS zinajumuisha ulinzi wa amani. Miaka ya 1990 nchi wanachama wa ECOWAS zilituma kikosi cha kulinda amani kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia na Sierra Leone.
ECOWAS pia iliingilia kati nchini Ivory Coast, Guinea-Bissau na Mali. Mnamo mwaka 2017 pale rais wa Gambia Yahya Jammeh alipokataa kukabidhi madaraka kwa mrithi wake aliyechaguliwa kidemokrasia, Adama Barrow, jumuiya ya ECOWAS ilituma wanajeshi.
Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, wanamgambo wa itikadi kali za kiislamu wameitikisa kanda ya Sahel na kutoa changamoto mpya kwa jumuiya hiyo.Operation nyingi za kimataifa zimeshindwa kutatua tatizo hilo na kuacha fadhaa miongoni mwa mataifa masikini ya kanda hiyo ya Mali, Burkina Faso na Niger.
Hali hiyo imechochea watawala wa kijeshi kunyakua madaraka kwenye mataifa hayo kati yam waka 2020 na 2023. Mwaka 2022, mataifa ya ECOWAS yaliafikiana kuunda kikosi cha kijeshi cha kanda hiyo. Hapo kabla vikosi vidogo vilivyounda na nchi moja moja wanachama wa ECOWAS mfano wa kundi la nchi tano za Sahel (G5), havikupata mafanikio ya maana.
Wataalamu tayari wametahadharisha kwamba bila ya kupatikana fedha za kutosha kikosi hicho kipya cha kikanda kimejitengenezea hatma ya kuwa chombo kisicho na makali.
"Suala siyo tu kuunda kikosi cha kijeshi, bali kukifanya kiwe na uwezo” amesema Abdoulaye Sounaye, mtafiti wa dini ya kiislamu kutoka taasisi ya elimu ya Leibniz.
Mwanazuoni huyo ameiambia DW kuwa jambo la maani ni kutathmini vipi "kikosi hicho kitafanya kazi, kitakuwa na uwezo gani kwenye medani ya vita na kitapata wapi fedha?". Anasema utegemezi wa michango kutoka nchi wanachama haujaonesha kuwa na matokeo yoyote kwa miaka yote.
Lakini ECOWAS inaweza kufanya nini hivi sasa?
Mzozo wa kanda ya Sahel kwa hakika ni mzozo unaoiathiri pia ECOWAS. Baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea, Mali na Burkina Faso sasa wanajeshi wamechukua pia madaraka nchini Niger.
Mkataba wa ECOWAS unatoa ruhusa ya chombo hicho kuweka vikwazo dhidi ya nchi wanachama katika mazingira kama hayo ya kuangushwa utawala wa kidemokrasi.
Jumuiya hiyo inaweza kuzuiia uhuru wa watu kusafiri baina ya mipaka ya nchi zilizofanya mapinduzi nan chi nyingine wanachama wa ECOWAS pamoja na kusitisha safari za ndege. Pia inaweza kufunga shughuli za ubadilishanaji fedha na mitaji kwenye kanda ya sarafu ya Faranga.
Na hatua nyingine nzito inayowezekana ni kusitisha kwa muda uanachama wa nchi iliyokutwa na balaa la mapinduzi. Hilo limetokea kwa nchini zote nne zilizofanya mapinduzi.
Mtaalamu wa sayansi ya jamii Bounty Diallo kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey, ameimbia DW kwamba vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS dhidi ya Mali na Burkina Faso vimeshindwa kutoa shinikizo lolote kwa tawala mpya za kijeshi wala kubadili fikra za raia wa mataifa hayo.
Msomi huyo amesema "kufikiri kuwa mambo yatakuwa tofauti kwa Niger na kwamba serikali ya kijeshi inatii amri ya kurejesha utawala wa kiraia ndani ya wiki moja, ni ndoto za mchana”