COP28: Mazungumzo kuhusu nishati ya visukuku yapamba moto
6 Desemba 2023Shinikizo la kupata ufanisi linaongezeka wakati mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi ya Umoja wa Mataifa yakikaribia kufika mwisho wa wiki yake ya kwanza huku rasimu ya hivi karibuni ya makubaliano ya kimataifa ya hali ya hewa ikitarajiwa leo kabla ya kukamilishwa mnamo Desemba 12. Haya ni kwa mujibu wa mwangalizi mmoja.
Simon Stiell ayataka mataifa kukoma kuoneshana ubabe
Mkuu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa Simon Stiell leo ameyaambia mataifa yanayoshiriki katika mkutano huo wa COP28 kukubaliana kuhusu hatua kabambe za kushughulikia ongezeko la joto duniani badala ya kuingia katika mtego wa kuonyeshana ubabe.
Hatima ya matumizi ya mafuta, gesi na makaa ya mawe, zinazochangia zaidi katika ongezeko la joto linalotokana na shughuli za binadamu, imekuwa suala kuu katika agenda ya mkutano huo wa COP28 na migawanyiko kuhusu hatma hiyo imedhihirika wazi katika kongamano hilo.
Soma pia:COP28 ipo katika tafakari kuachana na nishati ya visukuku
Jumanne (6.12.2023), mmoja wa washirika katika mazungumzo hayo alisema kwamba hali inabadilika badilika huku waakilishi wa takriban nchi 200 wakijadiliana kuhusu rasimu hiyo ambayo inajibu ukosefu wa ufanisi katika kupunguza ongezeko la joto.
Awali mvutano ulikuwa kuhusu iwapo kutakuwa na makubaliano ya kukatiza kabisa ama kwa hatua matumizi ya nishati ya visukuku.
Msemo mpya unaozingatia kukatiza matumizi ya nishati ya visukuku kwa mpangilio na haki huenda ukaashiria suala la makubaliano na kuzipa nchi tofauti muda tofauti wa kuzingatia kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kulingana na kiwango chao cha maendeleo na utegemezi wao nishati za uchafuzi wa mazingira.
India pia yapinga kutajwa kwa sekta maalumu au vyanzo vya nishati
Kulingana na waangalizi kadhaa wanaohudhuria mikutano ya faragha, kuna chaguo lingine, la kutotajwa kabisa kukatizwa kwa matumizi ya nishati ya visukuku ambalo linaonesha upinzani kutoka mataifa yanayozijumuisha Saudi Arabia na China. Muangalizi mmoja amesema kuwa hapo jana jioni, India pia ilipinga kutajwa kwa sekta maalum au vyanzo vya nishati.
Katika hatua nyingine Steiner, ameliambia shirika la habari la dpa kwamba bila shaka ni vigumu kwa watu wengi kuelewa kwanini Sultan al-Jaber, anaesimamia Kampuni ya mafuta ya Abu Dhabi - ADNOC ni rais wa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa huko Dubai.
Soma pia:COP28: Ahadi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi hazitekelezwi ipasavyo
Hata hivyo, Steiner amesema kuwa inaweza pia kutambuliwa kuwa nchi inayozalisha mafuta pia inakabiliana na changamoto iliyoko ya ongezeko la joto na inataka kuchangia katika makubaliano miongoni mwa mataifa hayo 200.
Steiner ametoa wito wa subira hadi mwisho wa kongamano hilo ili kutathmini jukumu la Umoja wa Falme za Kiarabu kama mwenyeji wa mkutano huo ikilinganishwa na matokeo ya mkutano huo.
Steiner amesema kuwa nchi za Magharibi pia ziko matatani linapokuja suala la uzalishaji wa mafuta. Alitoa mfano wa Marekani, Canada, Norway na Uingereza ambazo zote zimesema zinataka kupanua uzalishaji wao wa mafuta.