COP28 ipo katika tafakari kuachana na nishati ya visukuku
5 Desemba 2023Rasimu ya mazungumzo, iliyoonekana leo Jumanne, kuhusu mkutano wa kukabaliana na mabadiliko ya tabia nchi wa Cop28 inaonesha kwamba mataifa yanayoshiriki mkutano huo yanatafakari kutowa mwito wa kutangaza rasmi hatua ya kuachana kabisa na nishati ya visukuku. Kwa mujibu wa rasimu hiyo, hatua hiyo inapangwa kuchukuliwa kama sehemu ya makubaliano ya mwisho ya kupambana na ongezeko la jotoduniani katika mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Mataifa. Utafiti uliochapishwa leo unaonesha kwamba kiwango cha gesi ukaa inayozalishwa duniani kinatarajiwa kuvunja rekodi na kuchochea ongezeko kubwa la mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuchochea hali mbaya zaidi ya hewa. Maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, wameeleza kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa kiasi nchi 60 zinazounga mkono ahadi itakayotolewa leo ya kupunguza shughuli zinazosababisha utoaji wa gesi ukaa kufikia mwaka 2050.