Blinken kuzuru Afrika kujaribu kuweka mambo sawa
20 Januari 2024Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Blinken, atayatembelea mataifa hayo kuanzia Jumapili Januari 21 hadi 26 atakapopata pia nafasi ya kujadili kuhusu ushirika wa Marekani na Afrika katika masuala ya biashara, hali ya hewa, miundo mbinu na afya.
Masuala mengine yatakayotupiwa macho ni pamoja na usalama wa kikanda, kuzuia mizozo na kukuza demokrasia.
Nigeria, moja ya nchi atakazotembelea Blinken ni taifa lenye nguvu kubwa katika Ukanda wa Afrika ya Magharibi na ina nafasi kubwa katika masuala ya kiusalama hasa yale yanayohusisha machafuko yanayofanywa na makundi ya itikadi kali kwenye ukanda wa Sahel.
Changamoto za kiusalama zinazoisibu Afrika ya magharibi hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Niger zitajadiliwa Blinken atakapokuwa ziarani.
Msaidizi wa Blinken anayeshughulikia masuala ya Afrika, Molly Phee aliwaambia wanaandishi wa habari kuwa, Marekani ina historia inayofahamika na matumaini kuwa viongozi wa serikali ya kijeshi ya Niger itachagua kushirikiana na Washington badala ya Urusi.
Soma pia: Blinken: Marekani kutoa tangazo 'zito' kuiunga mkono Afrika
Msaidizi huyo wa Blinken ameongeza kuwa, iwapo watawala hao wa kijeshi watachagua kushirikiana na Urusi, mambo yatakuwa magumu.
Phee aliitolea mfano Mali ambapo amesema kumekuwa na ongezeko la majeruhi pamoja na mashambulizi ya kiusalama tangu serikali ya nchi hiyo ilipolikaribisha kundi la mamluki wa kijeshi wa kampuni ya Wagner ya Urusi.
Urusi yazidi kujiimarisha Afrika Magharibi
Wizara ya ulinzi ya Urusi mapema Jumanne ilisema kuwa nchi hiyo na Niger, zimekubaliana kuanzisha ushirikiano wa kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka uliopita.
Viongozi wa kijeshi wa Niger walivifukuza vikosi vya Ufaransa na kukatisha mikataba ya kiusalama na Umoja wa Ulaya hali iliyowaacha washirika wa mataifa ya magharibi kuhofia kuwa nchi hiyo huenda ikageuka kuwa ngome mpya ya Urusi katika ukanda huo.
Molly Phee amesema kuwa ziara ya Blinken barani Afrika ni sehemu ya ufuatiliaji wa mkutano uliofanyika Washington na kuhudhuriwa mna viongozi wa bara hilo mwaka 2022 ambapo rais Joe Biden aliahidi kuwa Marekani ko kwa ajili ya mustakabali wa Afrika.
Niger imekuwa mshirika muhimu wa Marekani katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali ambao wameshawauwa maelfu ya watu katika ukanda wa Sahel huko Afrika ya magharibi.
Suala jingine linalotarajiwa kuangaziwa kwenye safari hiyo ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani barani Afrika ni mivutano inayoendelea kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia: Wanaharakati wataka Blinken azingatia haki za binadamu katika safari Afrika
Blinken anaizuru Afrika wakati Marekani ikiwa na wasiwasi kuhusu uhusiano wake na bara hilo hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Niger na Gabon pamoja na machafuko yanayoendelea Sudan na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Atakapokuwa Ivory Coast, Antony Blinken huenda akahudhuria michuano ya kombe la mataifa ya Afrika katika mechi itakayochezwa kati ya taifa hilo mwenyeji na Equatorial Guinea.
Itakumbukwa kuwa Marekani na China, zimekuwa zikipambania kupata ushawishi kote barani humo. Mada hii huenda ikawa katika ajenda zitakazojadiliwa Blinken atakapofika Angola, nchi ambayo China inailenga katika kufanya uwekezaji muhimu.
Chanzo: APE/Reuters