1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Blinken: Marekani kutoa tangazo 'zito' kuiunga mkono Afrika

14 Desemba 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amekutana na rais wa Senegal Macky Sall, ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, wakati wa mkutano wa kilele kati ya Afrika na Marekani huko Washington.

https://p.dw.com/p/4Kvbg
USA Washington | US Afrika Gipfel
Picha: Evelyn Hockstein/AP/picture alliance

Waziri Anthony Blinken amesema alipokutana na Sall kwamba Senegal imekuwa mshirika muhimu sana wa Marekani katika masuala kadhaa kuanzia ya usalama, ujenzi wa uchumi, vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi hadi mapambano kuelekea changamoto za kikanda. Amesema ni muhimu sana kuendeleza majadiliano na uhusiano huo.

Blinken amefahamisha kuwa serikali ya Marekani inajiandaa kutoa tangazo zito siku ya Ijumaa wakati itakapotangaza kuunga mkono mpango wa kuufanya Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa kudumu wa kundi la mataifa yanayoendelea na yaliyoinukia kiuchumi la G20, hatua iliyopongezwa na rais Sall.

Soma pia: Marekani yatiwa wasiwasi na ushawishi wa China barani Afrika

"Nafurahishwa na kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili zetu hizi mbili ambao ni wa kipekee, na hasa ushiriki wa Marekani katika masuala makubwa katika ngazi ya kimataifa ya amani na usalama pamoja na changamoto zinazotukabili," alisema Rais Sall.

USA Washington | USA-Afrika-Gipfel | Ankunft Macky Sall, Präsident Senegal
Rais wa Senegal na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sall akiwasili Washington kuhudhuria mkutano wa kilele kati ya Marekani na Afrika, Desemba 12, 2022.Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

"Tayari nimeona rasimu ya tamko la mkutano huu, ambalo linatia moyo sana tunaposonga mbele na tunaliunga mkono kikamilifu. Napenda kupongeza nafasi ya kihistoria ya rais Joe Biden, na nadhani atathibitisha vile vile kuhusu kuupa Umoja wa Afrika nafasi ndani ya G20. Nadhani hii itasaidia kujenga ushirikiano imara zaidi na Afrika."

Masuala muhimu ya majadiliano

Mapema, waziri Blinken aliyataja masuala muhimu kwenye majadiliano na wakuu hao ambayo ni pamoja na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa Bonde la Kongo na wasiwasi ulioko kati ya Kongo na Rwanda, mashariki mwa taifa hilo, huku akionya kwamba China na Urusi zimekuwa zikilidhoofisha bara hilo kwa kuongeza ushawishi wake.

Soma pia: Kwanini bara la Afrika ni muhimu kimkakati ?

Hata hivyo China imekosoa madai hayo, huku balozi wake nchini Marekani Qin Gang akisema bara hilo sio eneo la kugombaniwa na mataifa makubwa. Ameitaka Marekani kuheshimu matakwa ya WaAfrika na kuchukua hatua madhubuti za kuisaidia badala ya kuendelea kuyashambulia mataifa mengine.

Hili ni kusanyiko kubwa kabisa na la kwanza la kimataifa mjini Washington tangu enzi ya rais Barack Obama mwaka 2014, huku mrithi wake Donald Trump akionyesha wazi kabisa kutokuwa na mpango na bara hilo.

Masuala ya usalama yamesalia kuwa kitovu cha mijadala kwenye mkutano huo, ambao rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi ameutumia kuiomba Marekani kuongeza mbinyo kwa Rwanda kufuatia machafuko mashariki mwa Kongo, akisema wao ndio waathirika wa uvamizi wa Rwanda inaoufanya kupitia mgongo wa waasi wa M23.

Chanzo: AFPE/APTN/EBU