1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aelekea Afrika

14 Machi 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani atarajiwa kuishinikiza Ethiopia kutekeleza makubaliano ya kusitisha vita kaskazini mwa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/4OflP
Indien | G20 Antony Blinken
Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anatarajiwa leo kuanza ziara nchini Ethiopia, ikiwa ziara ya kwanza ya mjumbe wa ngazi ya juu wa Marekani kuitembelea nchi hiyo tangu kumalizika vita katika jimbo la Tigray.

Tigray-Krise in Äthiopien
Picha: UGC/AP/picture alliance

Antony Blinken aliondoka Jumatatu usiku nchini Marekani kuelekea kwenye ziara yake barani Afrika itakayomfikisha Ethiopia hii leo na baadae nchini Niger.Akiwa Adis Ababa anatarajiwa kuhimiza juu ya mchakato wa amani.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Blinken atajadili suala la makubaliano ya amani yaliyomaliza vita kaskazini mwa nchi hiyo kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa chama kinachopigania ukombozi wa watu wa Tigray TPLF.

Aidha atakapokuwa nchini Niger anatarajiwa kujadili kuhusu juhudi za kupambana na ugaidi ambazo zinalenga kuyamaliza makundi ya itikadi kali katika nchi hiyo na katika eneo zima la Sahel kwa ujuma wake.

Ziara ya Blinken inakuja katika wakati ambapo Marekani inaonekana kuongeza juhudi za kujihusisha katika bara la Afrika kuukabili ushawishi wa China unaoongezeka kwenye bara hilo.

USA Washington | US Afrika Gipfel
Picha: Evelyn Hockstein/AP/picture alliance

Ziara hiyo ya Blinken itakuwa ni ya tatu ya kiongozi wa juu kutoka utawala wa rais Joe Biden katika bara hilo mwaka huu.

Viongozi wengine wa Marekani walioitembelea Afrika mwaka huu ni pamoja na waziri wa fedha Janet Yellen,balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa  Linda Thomas-Greenfield na mke wa rais Joe Biden Jill Biden.Aidha makamu wa rais Kamala Harris anatarajiwa pia kulitembelea bara hilo mwishoni mwa mwezi huu wa March akitarajiwa kwenda Ghana,Tanzania na Zambia katika ziara ya wiki moja.

Antony Blinken anapanga kukutana na viongozi wa Ethiopia na maafisa wa Tigray mjini Addis Ababa na mazungumzo yake na waziri mkuu Abiy Ahmed na maafisa wa Tigray yatatuwama zaidi katika suala la utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha vita kwa ajili ya kuendeleza amani na kuunga mkono juhudi za kupatikana haki kaskazini mwa Ethiopia baada ya mgogoro.

Vita katika jimbo hilo vilisababisha Marekani  kusitisha baadhi ya makubaliano ya kibiashara na Ethiopia ambayo nchi hiyo inataka yarudishwe.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa und Blinken
Picha: Andrew Harnik/AP/picture alliance

Hata hivyo siku ya Ijumaa mwanadiplomasia  wa ngazi ya juu wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika Molly Phee, alisema ili kurudisha mahusiano kamili ya kawaida na nchi hiyo itategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya mjini Addis Ababa na hasa baada ya mgogoro huo wa Tigray.

Kiasi watu 500,000 waliuwawa katika mgogoro uliodumu kwa  miaka miwili na ambao ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini nchini Afrika Kusini mwezi Novemba baada ya maafisa wa Marekani kusimamia juhudi hizo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW