Blinken azungumza na Kagame na Tshisekedi kuhusu M23
7 Novemba 2023Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Blinken alizungumza kwa simu na kwa nyakati tofauti na marais Felix Tshisekedi wa Kongo na Paul Kagame wa Rwanda kuhusu hali isiyo tulivu kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Matthew Miller, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, amesema Blinken alipendekeza suluhu la kidiplomasia kwa mvutano kati ya Kongo na Rwanda na kuhimiza kila upande kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wanajeshi kwenye mpaka.
Waasi wa M23, wanaopigana jimboni Kivu ya Kaskazini linalopakana na Rwanda, wamezidisha mashambulizi tangu mwezi uliopita, huku Umoja wa Mataifa ukiripoti kuwa watu wengine laki mbili wamekimbia makazi yao.
Baada ya kuzuka kwa mapigano baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23, mwaka jana , Blinken alitembelea Kongo na Rwanda. Aliunga mkono hadharani madai ya Kinshasa kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23. Serikali ya Kagame inakanusha madai hayo.
Kongo yataka vikwazo dhidi ya Rwanda
Huku hayo yakijiri, vita vya maneno viilibuka upya baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo kwenye mkutano wa mawaziri wa nchi zinazozungumza kifaransa mjini Yaoundé, Cameroon. Kwenye hafla hiyo, Crispin Mbadu, naibu waziri wa mambo ya nje wa Kongo alizitaka nchi wanachama wa Francophonie kuichukulia hatua kali Rwanda katika kile alichosema kuwa ni ungwaji mkono wa wazi wa viongozi wa Rwanda kwa waasi wa M23 huko Kivu ya Kaskazini.
''Rwanda kisingizio kwa kila jambo''
Bila kusita, Vicent Biruta waziri wa mambo ya nje wa Rwanda alijibu tuhuma hizo na kusema mzozo wa Kongo ni baina ya wakongo wenyewe.
''Katika majukwaa yote ya kimataifa Kongo imeyatumia hivi sasa kuishutumu Rwanda, baada ya viongozi wake kushindwa kuboresha utawala mbaya ambao ni sifa ya nchi hii. Lakini pia Kongo imeamua kuyaweka nje matatizo yake ya ndani na kuichagua Rwanda kuwa kisingizio kwa kila jambo ambalo haliendi sawa nchini Kongo.'', alisema Biruta.
Juhudi zote za kikanda za kutaka kutatua mzozo huo baina ya Kongo na Rwanda bado kufanikiwa.
Umoja wa Mataifa umesema umerekodi wakimbizi wa ndani milioni 6.9 kote nchini Kongo wengi wao kutokana na ghasia za hivi sasa mashariki mwa nchi hiyo.