Mapigano yaibuka Kongo kati ya M23 na vijana wazalendo
25 Oktoba 2023Vyanzo kutoka kwa mashirika ya kiraia vimeelezea kuwa ni waasi wa M23 ndio walirushia makombora ngome za jeshi la serikali ya Kongo huku waasi hao wanaodaiwa kusaidiwa na jeshi la Rwanda wakijibu mashambulizi ya muungano huo wa vijana wazalendo wanao saidiwa na serikali ya Congo.
Mapigano hayo yaliyofuatiwa na kifo cha mwanajeshi kutoka jeshi la kikanda,EAC mwenye uraia wa Kenya , yalianza mchana baada ya utulivu wa muda kati ya saa moja na saa nne unusu kwenye kijiji cha Buhumba wilayani Nyiragongo.
Soma pia: Waasi wa M23 waudhibiti mji wa kimkakati wa Kitshanga
Vyanzo kadhaa vilithibitisha kuwa waaasi wa M23 walikuwa wakirusha mizinga kutoka mlima Kanyabuki chini ya mlima Nyiragongo kuelekea ngome za jeshi la FARDC mita chache tu kutoka kambi ya kikosi cha Kenya.
Hata hivyo, katika tangazo lao jana jioni, Luteni Kanali Guillaume Ndjike msemaji wake gavana kijeshi Kivu Kaskazini ,alisema kuwa jeshi la serikali FARDC ililazimika kujibu shambulio hilo ili kuwazuiya waasi hao walio anza kuelekea katika eneo la Rusayo nje kidogo na mji wa Goma ambako hali ya wasiwasi ilitanda siku nzima.
Asasi za kiraia zalizaka jeshi kuwadhibiti waasi wa M23
Wakati huohuo ,asasi za kiraia zimelitaka jeshi tiifu kwa serikali ya Congo kukabiliana mara moja na waasi wa M23 kabla yao kuwashawishi raia kuingilia kati.
Hadi kufikia mida ya jioni ,waasi wa M23 walikuwa wanaendelea kuzilenga ngome za FARDC kwenye mlima Kanyabuki ambako walitimuliwa na muungano wa vijana wazalendo wanaoungwa mkono na jeshi la kongo katika mapigano hayo yanayoingia wiki yake ya tatu sasa.
Soma pia:Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke DRC
Siku moja kabla,ya juma tatu oktoba 23 serikali ya kongo iliwashutumu waasi wa M23 kwa kuwauwa raia karibu na eneo la Tongo wilayani Rutshuru, madai ambayo kundi hilo lilikanusha.
Serikali ya Kongo pia ilichapisha picha zilizoonyesha msafara wa wanajeshi wa Rwanda wakiingia kivu kaskazini kupitia mbuga ya Virunga.