1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya ushindi, Tshisekedi anao mlima mrefu wa kupanda

Saleh Mwanamilongo
4 Januari 2024

Felix Tshisekedi ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Desemba 20 uliogubikwa na utata. Lakini njia ya muhula wake wa pili madarakani imejaa viunzi virefu.

https://p.dw.com/p/4aoze
DR Kongo Felix Tshisekedi in Kinshasa
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Kwenye mkesha wa mwaka mpya, Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, CENI ilimtangaza Rais Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa tarehe 20 Desemba 2023. Ingawa kwa mujibu wa matokeo hayo ya awali  kiongozi huyo alipata ushindi wa kishindo wa asilimia 73.34, ikiwa atathibitishwa na Korti ya Katiba, ataanza muhula wa pili akikabiliwa na changamoto lukuki, katika sekta za usalama, utangamano wa kitaifa na wa kikanda, na uchumi uliosambaratika.

Alipochaguliwa kuongozi muhula wa kwanza, Felix Tshisekedi aliahidi kumaliza machafuko ambayo yamekuwa kama donda-ndungu katika eneo la mashariki mwa nchi yake hususan katika mkoa wa Kivu Kaskazini, kwa kauli ya ‘‘niko tayari kujitolea uhai wangu ili amani irejee.‘‘ Miaka mitano baadaye, hali ni mbaya zaidi kuliko alivyoikuta.

Waandamajani 10 wamejeruhiwa nchini DRC

Waasi wa kigeni na wakimbizi wa ndani

Tofauti na awali ambako makundi yenye silaha yapatayo 200 katika eneo hilo hayakuwa na malengo ya kisiasa, hivi sasa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limeyakamata maeneo makubwa, likitishia kuukamata mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma wenye wakaazi zaidi ya milioni moja.

Yapo pia makundi yenye asili ya nchi za nje, kama The Allied Democratic Forces (ADF), kutoka Uganda, na The Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR). Mashambulizi ya umwagaji damu yanayofanywa na makundi hayo dhidi ya raia , yamewafanya mamia ya maelfu kuyapa kisogo makaazi yao.

‘'Leo hii tuna idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kuliko wakati mwingine wowote nchini DRC huku karibu watu milioni 7 wakiwa wameyahama makazi yao kutokana na hali ngumu ya usalama,'' aliiambia DW, Jason Stearns, mkurugenzi wa Shirika la Utafiti kuhusu Kongo (GEC) la Chuo Kikuu cha New York.

''Kwa sasa haiwezekani kufikiria utulivu wa muda mrefu huko mashariki bila kuimarisha uwajibikaji wa serikali.'', alitahadharisha mtafiti huyo raia wa Marekani, na kuongeza kuwa Tshisekedi anatakiwa kuanzisha mageuzi ya kina yatakayorahisisha kuyapokonya silaha makundi yote ya wapiganaji.

Wanajeshi wa Kongo na Uganda waendesha operesheni za pamoja jimboni Kivu ya Kaskazini dhidi ya waasi wa ADF
Wanajeshi wa Kongo na Uganda waendesha operesheni za pamoja jimboni Kivu ya Kaskazini dhidi ya waasi wa ADF Picha: Alain Uaykani/Xinhua/IMAGO

Wito kama huo umetolewa pia na Yvon Muya, Mhadhiri katika taasisi ya utatifi wa migogoro kwenye Chuo Kikuu cha Saint-Paul nchini Canada  ambaye  anasema Tshisekedi atatakiwa kulifanya suala la usalama kuwa lenye kipaumbele zaidi.

‘'Atalazimika kutoa majibu ya haraka au, angalau, kuwaonyesha Wakongo kwamba ana mkakati wa kuaminika katika kukabiliana na mzozo wa mashariki ambao umefikia katika kiwango kibaya kabisa.'' alisema Muya katika mahojiano na DW.

Karte DR Kongo EN

Uadui wa kisiasa unaotishia umoja wa kitaifa

Uchaguzi wa Desemba 2023 uliitishwa katika mazingira ya kutoaminiana baina ya washirika ambao ni wanasiasa na asasi za kiraia likiwemo Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa katika siasa za Kongo. Baada ya kutengena na mtangulizi wake Joseph Kabila aliyeongoza kati ya 2001-2018, Tshisekedi aliimarisha madaraka yake kwa kuwateuwa majaji wa Mahakama ya Katiba na viongozi wakuu jeshini.

Wagombea wakuu walipinga uongozi wa tume ya uchaguzi na kuituhumu kuundwa mahsusi kumpa ushindi Tshisekedi. Kampeni ya uchaguzi ya mwezi mzima ilisheheni kauli za chuki zenye msingi wa kikabila, na wachambuzi wanasema Tshisekedi atapaswa kutafuta haraka mbinu za kuliunganisha tena taifa lililogawika.

‘'Itambidi sasa kutafuta maneno ya kujenga jamii na kumfanya kila Mkongo ajihisi kuwa ni raia wa taifa moja,'' alisema Yvon Muya wa Chuo Kikuu cha Saint-Paul.

Kongo ilishuhudia kampeni ya uchaguzi iliojaa jumbe za chuki, ubaguzi na ukabila
Kongo ilishuhudia kampeni ya uchaguzi iliojaa jumbe za chuki, ubaguzi na ukabilaPicha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Haitakuwa kazi mteremko, kwa sababu kando na wapinzani rasmi wa kisiasa wanaopania kuuhujumu utawala wake kwa maandamano ya muda mrefu, umezinduliwa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi wa Alliance Fleuve Congo (AFC), chini ya uongozi wa Corneille Nangaa, mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, CENI, anayetishia kumng'oa Tshisekedi kwa mtutu wa bunduki.

Mvutano wa kikanda unaozidi kutanuka

Katika muhula wake mpya, Rais Felix Tshisekedi anakabiliwa na kibarua kigumu cha kusuka mkakati mpya wa ushirikiano wa kikanda, kufuatia kutanuka kwa ufa baina ya utawala wake na nchi washirika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Juu ya Rwanda ambaye ni hasimu wa jadi wa Kongo-Kinshasa, kutoelewana juu ya majukumu ya kikosi cha jumuiya hiyo katika kupambana na waasi wa M23, kumesababisha mgongano baina ya Kinshasa na Nairobi, huku Kampala pia ikihusishwa na njama dhidi ya Kongo, japo sio kwa njia za wazi wazi.

‘'Ufumbuzi wa suala la usalama mashariki utahitaji utulivu kati ya nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa vyovyote vile, ikiwa ni lazima kujadiliana na viongozi halisi wa M23, serikali ya Kongo inajua kwamba lazima ifanye upya mazungumzo na Rwanda.'', alieleza Yvon Muya katika mahojiano na DW.

Uhusiano baina ya Kongo na Rwanda umekuwa wa panda shuka kwa takriban miaka 30 sasa
Uhusiano baina ya Kongo na Rwanda umekuwa wa panda shuka kwa takriban miaka 30 sasaPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Tshisekedi alitumia muda mwingi wa muhula wake wa kwanza kwenye safari za nje ili kupalilia uhusiano bora na nchi jirani na kuwavutia wawekezaji wa nje bila mafanikio makubwa. Juhudi zake za kidiplomasia zilikwamishwa na kashfa nyingi za rushwa zilizowaandama watu wake wa karibu na  maafisa waandamizi wa serikali yake.

Nchi Tajiri, raia masikini

Rais Felix Tshisekedi aliwahi kuahidi kwamba  ataigeuza Kongo kuwa kama ‘'Ujerumani ya Afrika''. Kinyume na ahadi hiyo, chini ya utawala wake thamani ya faranga ya Kongo imezidi kuporomoka, hali ambayo imedidimiza kiwango cha ubora wa maisha kwa wananchi walio wengi. Wakati wa kampeni yake ya uchaguzi kadhia ya kupanda kwa gharama ya maisha ilikuwa midomoni mwa wananchi waliohudhuria mikutano yake.

Ukosefu wa ajira kwa raia wengi hasa vijana, ni kilio kilichohanikiza kila mahali alipopita.

Licha ya utajiri wa madani kwenye ardhi yao, Wakongo waliowengi wanaishi chini ya mustari wa umasikini
Licha ya utajiri wa madani kwenye ardhi yao, Wakongo waliowengi wanaishi chini ya mustari wa umasikiniPicha: Federico Scoppa/AFP/Getty Images

Katika lugha tamu ya kampeni Tshisekedi alisema ataunda nafasi za kazi zipatazo milioni 6.2 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Aidha, aliahidi kudhibiti mfumko wa bei, ambao kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia uko katika kiwango cha asilimia 20.7, huku ukuwaji wa uchumi mnamo mwaka wa 2023 ukiwa wa asilimia 6.8.

Israel Mutala, mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini Kongo anasema ukuaji wa Kongo unapaswa kuwa wa zaidi ya asilimia 10, na kulifikia lengo hilo ni changamoto nyingine inayomkodolea macho Tshisekedi katika muhula wake mpya.

‘'…pia kuutanua uchumi ili usitegee tu sekta ya madini, kwa kujumuisha kilimo na ujenzi wa miundombinu ya nishati, na njia za usafiri wa ardhini hasa barabara na reli,'' alishauri Mutala.

Msingi katika sekta ya huduma za jamii

Pembeni mwa mkururo wa ahadi ambazo alishindwa kuzitimiza, Rais Tshisekedi anaweza kujivunia sera ya utoaji wa elimu ya msingi ya bure na hivi karibuni mpango wa akina mama kujifungua bila malipo katika hospitali za umma. Sera hiyo inaonekana kuwa nembo moja ya mafanikio muhimu ya mpango wake kwa kijamii ambayo aliyanadi katika kampeni yake ya uchaguzi kwa ajili ya muhula wa pili. 

Lakini kauli mbiu ya "Le peuple d'abord" ama‘‘umma kwanza‘‘ ambayo iliasisiwa na chama chake cha UDPS (l'Union pour la démocratie et le progrès social), ambayo ililenga kuwakomboa raia wa Kongo milioni 20 kutoka katika lindi la umasikini wa kupindukia, imeishia kuwa ndoto ya alinacha. 

Raia wanasubiri kuona matokeo ya kauli mbiu ya  ''Umma Kwanza'' ya chama cha UDPS
Raia wanasubiri kuona matokeo ya kauli mbiu ya ''Umma Kwanza'' ya chama cha UDPSPicha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Israel Mutala ili kufanikiwa kiuchumi, Tshisekedi hatakuwa na budi kubadilisha dira yake kidiplomasia.

‘'Mbali na diplomasia ya vita au amani, tunahitaji diplomasia ya maendeleo ambayo inawavutia wawekezaji wengi wa kigeni. Diplomasia ya mitaji ya kimataifa itakayowezesha kugharimia miradi ya kimuundo'', mtaalamu huyo wa uchumi aliiambia DW.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo robo ya idadi ya watu wote wanakabiliwa na dharura ya hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula na asilimia 62 wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Ni asilimia 15 tu ya raia wa Kongo ambao wanayo huduma ya umeme, kioja ukizingatia kuwa nchi hiyo inalo bwawa la Inga, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 40,000 za nishati hiyo, kiwango ambacho ni takribani theluthi moja ya mahitaji ya nishati ya umeme kwa bara zima la Afrika.