Mtawa wa Kikongo anufaika na kiwanda chake cha umeme
29 Aprili 2022Serikali imefanya kazi na washirika wa kigeni ili kuinua uchumi wa taifa hilo lenye utajiri wa madini. Lakini pamoja na ufadhili wa mamilioni ya dola kwa nchi hiyo, ni asilimia 20 tu ya idadi ya watu ndio hupata umeme, kulingana na Benki ya Dunia.
Alphonsine Cize ni mwanamke anayetumia muda mwingi kwenye kiwanda cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji alichokijenga ili kuondokana na adha ya kukatika kwa umeme kila siku kwenye mji wa Miti uliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Anashirikiana na timu ya wahandisi kusimamia mtambo ili kusambaza umeme kwenye nyumba ya watawa, kanisani, shule mbili na zahanati bila malipo.
Bila mtambo huo, wakaazi wa hapo wangekuwa na umeme kwa masaa machache kwa siku mbili au tatu kwa wiki.
Anasema alichoshwa na kutegemea mwanga wa mishumaa na nishati yenye gharama kubwa ya mafuta ya jenereta, ndipo akaanza kuchangisha pesa mnamo mwaka 2015 ili kujenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji.
Alipata ujuzi huo kama mtawa mwenye umri mdogo, alipokuwa akishughulkia sehemu zenye hitilafu ya umeme kwenye nyumba ya watawa, ambapo aliwashawishi viongozi wake kumpeleka kusoma fani ya uhandisi wa mitambo.
Ilichukuwa nyumba ya watawa ya Ciza miaka mitatu kukusanya dola za Kimarekani 297,000 zilizohitajika kujenga mtambo ambao unazalisha takribani megawani moja ya umeme.
Ni kutokana na juhudi za Ciza, sasa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Maendeleo iliyopo mji wa Miti wanaweza kujifunza ujuzi wa kompyuta.
"Hapo awali, mara nyingi umeme ulikuepo usiku tu, wakati watoto hawapo shuleni ," mwalimu mkuu Mweze Nsimire Gilberte alisema, akiongeza kwamba kwa kuwa na mtambo wao wenyewe, "sasa kumeleta ahueni kubwa."
Neema Misheki
reuters