Upinzani na waangalizi watoa hadhari kuelekea uchaguzi Kongo
15 Desemba 2023Miongoni mwa hizo ni kadi za wapigakura zisizosomeka, kuzuiwa kwa ndege za baadhi ya wagombea wakati wa kampeni na kucheleweshwa kwa orodha za wapigakura.
Kwa miezi kadhaa, tume huru ya uchaguzi ya Kongo imekuwa ikipuuza wakosoaji wanaoituhumu kushindwa kuandaa uchaguzi ulio huru na wa haki kama ilivyoahidi, hata wakati huu inapokiri kuwa inakabiliwa na changamoto za usafirishaji wa vifaa katika maandalizi yake.
Wiki za mwisho za kampeni zimegubikwa na mivutano, ambapo wapinzani wa rais wa sasa Felix Tshisekedi wanalalamikia mazingira yasiwaruhusu usawa wa kwa wagombea wote.
Malalamiko yao yanahusisha shutuma kwamba serikali inataka ushindi kwa njia zote zikiwemo za udanganyifu, kama anavyolalama hapa Moise Katumba, mmoja wa wapinzani wakuu wa rais Felix Tshisekedi katika uchaguzi huu.
''Nimezuiliwa kufanya kampeni katika Kongo ya Kati, ndege ambazo nimetumia fedha nyingi kuzilipia zimekwama Afrika Kusini. Niliazimia kuwa na angalau ndege tisa, lakini sasa nakodi ndege nyingine. Hatusikii chochote kutoka kwa mamlaka ya ndege za safari, ambayo najua ni shirika lenye ustaarabu, lakini sasa linatumiwa.''
CENI yapuuza tuhuma zinaikabili kuelekea uchaguzi wa Disemba 20
Tume ya uchaguzi, CENI inasema shutuma hizo hazina msingi wowote.
Lakini kilicho hatarini sio tu uhalali wa uchaguzi wenyewe, bali pia amani ya nchi, kwa sababu malumbano juu ya matokeo ya uchaguzi, aghalabu huishia katika vurugu nchini Kongo.
Na zitokeapo ghasia sio Kongo tu inayoathirika, bali huwa na athari pana zaidi ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ndio mzalishaji mkubwa wa madini ya Cobalt, muhimu kwa utengenezaji wa batiri za magari ya umeme na simu za kiganjani.
Moise Katumbi, ambaye utajiri wake mkubwa unatokana na madini, anaonekana kama mpinzani muhimu zaidi dhidi ya rais Tshisekedi, katika orodha ya wagombea zaidi ya 20 wanaowania urais.
Wagombea wengine wa upinzani walia na ´rafu´wakati wa kampeni
Mbali na Katumbi anayelalamikia kuzuiwa kwa ndege zake, wagombea wengine wasio na uwezo mkubwa kifedha pia wanasema wamewekewa vizingiti katika kupeleka kampeni zao kwa wapigakura.
Barabara mbovu za Kongo ambazo ni mbaya zaidi mnamo majira haya ya mvua zimeyafanya mambo kuwa magumu zaidi.
Daktari Denis Mukwege ambaye ni mgombea mwingine maarufu, hivi karibuni alichapisha taarifa akiishutumu serikali kumkwamisha kwa kuchanachana mabango yake ya kampeni, na kubana upatikanaji wa mafuta ya ndege ili kuzuia safari za wapinzani.
Msemaji wa serikali ya mjini Kinshasa Patrick Muyaya ametupilia mbali shutuma zote hizo, akisema wapinzani wanajaribu kujionyesha kama wahanga.
Muyaya amesema hawahusiki katika alichokiita ''mchezo wa kutafuta mafanikio kwa kuwawekea wengine vizuizi.''