AU: "Uchaguzi Zimbabwe ulikuwa wa haki"
2 Agosti 2013Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe bado hayajatolewa lakini Rais Robert Mugabe anaamini kwamba ataibuka mshindi. "Inatarajiwa kwamba rais Mugabe atashinda kwa asilimia 70 mpaka 75," alisema Rugare Gumbo, msemaji wa chama tawala cha ZANU-PF.
Waangalizi wa Umoja wa Afrika wamesema Ijumaa kuwa kwa mtazamo wao uchaguzi wa Zimbabwe ulikuwa wa kuaminika na wa haki. Hata hivyo waangalizi hao wamekiri kwamba pamekuwa na hitilafu katika daftari la wapiga kura na baadhi ya wapiga kura ambao hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya uchaguzi.
Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ambaye ni mpinzani wa karibu zaidi wa Mugabe, amekosoa hitilafu hizo vikali na kusema kwamba uchaguzi si halali wala wa haki. "Haimaanishi kwamba SADC na Umoja wa Afrika ndio vigezo vya kimataifa vya uchaguzi wa huru na wa haki," alisema Tsvangirai. "Niseme pia kwamba licha ya vikwazo tulivyokumbana navyo, baadhi yetu tuliamini kwamba uchaguzi huu ungesuluhisha matatizo ya kiuchumi na ya kisiasa hapa Zimbabwe." Tsvangirai ameendelea kusema kwamba raia wa Zimbabwe watalazimika kubeba athari za maamuzi ya kisiasa na kicuhumi yaliyofanywa na Mugabe na ZANU-PF.
"Wamarekani wanataka tubatilishe uchaguzi"
Msemaji wa chama hicho, Rugare Gumbo ametupilia mbali shutuma za wizi wa kura. "Ni uongo mtupu. Tutawezaje kuiba kura? Huu ni mpango wa kubatilisha uchaguzi. Wamarekani na Waingereza wanataka tubatilishe uchaguzi," alisema Gumbo. "Hicho ndicho chanzo cha mambo yote haya. Ni jambo linalofadhiliwa na watu wengine."
Kwa upande wake, tume ya uchaguzi ya Zimbabwe nayo imesema kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na wa haki, licha ya hitilafu za hapa na pale. Akizungunza na DW, mwenyekiti wa tume hiyo, Solomon Zwana, alisema kwamba iwapo kuna chama ambacho hakijaridhika na matokeo, basi kinaweza kufuta njia za kisheria: "Tunatumaini kwamba vyama vitaheshimu ahadi walizoweka kwamba watafuata njia za kisheria na si kuanzisha virugu. Hilo ndio tumaini letu na ujumbe wetu kwa washika dau wa kisiasa." Mpaka kufikia jumatatu ijayo tume ya uchaguzi inapaswa iwe imetoa matokeo rasmi ya uchaguzi.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Columbus Mavhunga/dpa/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman