Polisi Zimbabwe yaonya watakaotangaza matokeo
1 Agosti 2013Kawaida, wakusanyaji matokeo vituoni huweza kutuma matokeo hayo kwa watu wengine, ikiwemo kupitia ujumbe mfupi wa simu za mikononi, na mitandao ya Intaneti, lakini safari hii msemaji wa polisi, Charity Charamba, amewaambia waandishi wa habari, yeyote atakayefanya hivyo atakamatwa.
Onyo hilo la polisi linafuatia mipango ya baadhi ya makundi ya kiraia kuchapisha matokeo ya uchaguzi kama yanavyopokelewa kutoka vituoni, kabla ya kuthibitishwa na kutangazwa rasmi na Tume ya Uchaguzi, kwa lengo la kuzuia wizi wa kura. Polisi inasema hatua yoyote ya aina hiyo ni kosa.
Ni amri itakayokiukwa
Hata hivyo, kuna uwezekano mdogo wa amri hiyo ya polisi kuheshimiwa hasa na mitandao ya kijamii, ambapo watu na taasisi nyingi zimejipanga kuyachapisha matukio na matokeo ya uchaguzi huo kama yatakavyoripotiwa.
Gazeti la The Guardian la Uingereza na Mail and Guardian la Afrika ya Kusini, ambalo mchapishaji wake ni raia wa Zimbabwe, yametengeneza ukurasa wa mtandaoni ambao utakusanya matokeo ya awali ya kura ya urais. Gazeti hilo limehoji kwamba matokeo ya awali hayamaanishi kutangaza ushindi wa mgombea au chama chochote cha siasa.
Nalo kundi la kupigania demokrasia nchini Zimbabwe liitwalo Sokwanale limetengeneza ramani ya matokeo ya uchaguzi, ambapo mtandao wa ZimDecides limeweka programu inayoripoti matukio yanayotilika mashaka kwenye vituo vya kupigia na kuhesabia kura. Afisa wa ngazi za juu wa Mtandao wa Kusaidia Uchaguzi nchini Zimbabwe, Frances Lovemore, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba tayari polisi imeanza kuwazuia watu kwenye vituo vingi vya kura na msako unaendelea.
Wengi wajitokeza kupiga kura
Wachambuzi wa siasa za Zimbabwe wanalihusisha onyo la polisi na kauli ya Rais Mugabe hapo Jumapili, kwamba angelimkamata hasimu yake, Tchangirai, kama angelijitangazia ushindi. Tchangirai alikuwa amesema kwamba chama chake kitatangaza matokeo ya uchaguzi mapema ikiwa tume ya uchaguzi itachelewa kufanya hivyo.
Wazimbabwe wengi walijitokeza kwa amani kupiga kura zao, tafauti na chaguzi zilizopita, na katika baadhi ya vituo walikaa hadi jioni sana, ambapo muda ulilazimika kuongezwa. Sasa wengi wao wanataka kujua matokeo ya kura zao, ambayo wanaamini yatafungua milango kwa misaada ya wafadhili wa Magharibi, inayohitajika sana kuufufua uchumi wa nchi hiyo.
Kila mmoja ajitabiria ushindi
Mugabe, mwenye umri wa miaka 89, ambaye anakanusha kwamba aliiba kura kwenye chaguzi zilizopita, amesema ana uhakika wa ushindi, lakini pia ameahidi kukubali kushindwa kama hilo litatokea.
Tchangirai naye amejitabiria ushindi mkubwa, zaidi ya ilivyokuwa kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi wa mwaka 2008, ambapo alimpita Mugabe, lakini si kwa wingi wa kutosha kuweza kutangazwa mshindi wa moja kwa moja. Wakati huo, Tchangirai aligomea uchaguzi wa marejeo, na hivyo kumpa fursa Mugabe ya kupita bila upinzani.
Kiasi cha watu milioni 6.4, ambao ni sawa na nusu ya raia wote wa Zimbabwe, walijiandikisha kupiga kura. Matokeo rasmi yanatarajiwa ndani ya kipindi cha siku tano, muda uliowekwa kuzuia uwezekano wa kurejelewa kwa matatizo yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa 2008, ambapo ucheleweshaji mkubwa ulichochea machafuko.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba