1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi utakuwa huru na haki asema Mugabe

MjahidA29 Julai 2013

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ametoa wito wa kuwepo amani katika uchaguzi mkuu ujao huku akiapa kuwa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika siku ya JJumatano wiki hii, utakuwa wa huru na haki.

https://p.dw.com/p/19Fl7
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: AP

Pigeni kura kwa amani alisema Rais Mugabe alipokuwa anawahutubia wafuasi wake takriban 40,000 katika kampeni zake za mwisho zilizofanyika kwenye uwanja wa taifa wa michezo mjini Harare jana .

Mugabe amesema bado mpaka sasa hakujashuhudiwa ghasia zozote katika siku za mwisho za kampeni ikilinganishwa na mwaka wa 2008.

Rais Robert Mugabe na Waziri wake Mkuu Morgan Tsvangirai
Rais Robert Mugabe na Waziri wake Mkuu Morgan TsvangiraiPicha: picture alliance/dpa

Aliwaambia waandishi habari kwamba uchaguzi utakuwa huru na haki kwa kuwa wapiga kura hawataelekezwa kupigia kura upande wowote, watachagua wenyewe ni nani atakayewaongoza tena.

Katika uchaguzi wa mwaka 2008 Tsvangirai alishinda katika maeneo mingi kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi iliojawa na ghasia lakini baadaye akajiondoa katika duru ya pili baada ya takriban wanachama 200 wa upinzani kuuwawa.

Mwaka mmoja baada ya uchaguzi huo Tsvangirai na Mugabe wakaunda serikali ya muungano.

Raia wa Zimbabwe kupiga kura wiki hii

Sasa raia wa Zimbabwe siku ya Jumatano watamchagua rais wao pamoja na bunge jipya ikiwa ni miaka minne baada ya Mugabe aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 34 kulazimika kugawana madaraka na waziri mkuu Morgan Tsvangirai.

Hata hivyo Rais huyo aliye na umri wa miaja 89 ameonya dhidi ya mataifa ya kigeni kuingilia uchaguzi wa nchi yake akiangazia tawala zilizoangushwa baada ya maandamano nchini Misri na Libya.

" Unaona kinachotokea Misri ni kwasababu walidanganywa ili wamuondoe rais wao, raia huko wanapigana huku mataifa ya Magharibi yakitazama tu ni kana kwamba hawajui walichokifanya katika nchi hiyo," Alisema Robert Mugabe.

Raia wa Zimbabwe katika chaguzi zilizopita
Raia wa Zimbabwe katika chaguzi zilizopitaPicha: picturr

Uhusiano kati ya Zimbabwe na mataifa ya Magharibi bado inabakia kuwa tete kufuatia vikwazo vya kimataifa ilivyoekewa nchi hiyo tangu mwaka wa 2002.

Kando na Mugabe kuwa katika kinyan'ganyiro cha kuwania muhula mwengine, amewaambia waandishi habari kwamba hata mwaka wa 2018 atakuwa katika mbio hizo hizo za kutaka kuiongoza nchi hiyo.

Morgan Tsvangirai afanya kampeni za mwisho

Kwa upande wake Waziri mkuu Morgan Tsvangirai anafanya kampeni zake za mwisho katika ukumbi mkubwa ulioko karibu na makao makuu ya chama cha ZANU-PF siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi huo mkuu.

Wakati huo huo afisa mkuu wa chama cha MDC cha waziri mkuu, alikamatwa jana kwa madai ya kuripoti wizi wa kura katika kura za mwazo zilizopigwa nchini humo ambazo ni za maafisa wa polisi na jeshi.

Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai
Waziri Mkuu Morgan TsvangiraiPicha: picture-alliance/dpa

Chama hicho kimesema Morgan Komichi alikamatwa baada ya kuripoti kwa tume ya uchaguzi kuwa karatasi za kupigia kura zilizokuwa na kura za chama hicho zilitupwa.

Polisi nchini humo sasa wametishia kumfungulia mashtaka Komichi kwa kuingilia sheria za tume ya uchaguzi iwapo hatasema ni nani aliyempa taarifa hizo za kutupwa kwa karatasi hizo za kupigia kura, zuilizokuwa na kura za MDC.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman