Uchaguzi mkuu wafanyika Zimbabwe
31 Julai 2013Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi kwa saa za Zimbabwe. Watu wengi waliwahi mapema na kupanga foleni mbele ya vituo wakiwa wamevaa sweta na makoti mazito kwa ajili ya kujikingia na baridi. Masaa manne baada ya vituo kufunguliwa, watu wengi waliofika mapema sana bado walikuwa hawajapata nafasi ya kuingia katika vituo vya kupgia kura.
"Tunasubiri hapa kuanzia saa moja na nusu asubuhi mpaka sasa hivi. Mambo yanakwenda taratibu sana. Sijui ni nini kinachoendelea huko ndani. Tungekuwa na vituo vingi zaidi labda mambo yangekwenda haraka zaidi. Tumechoka kusimama katika foleni," alisema mpiga kura huyo.
Shutuma za wizi wa kura
Takriban raia milioni 6.4 wana haki ya kupiga kura leo. Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe imekiri kwamba pamekuwa na hitilafu katika maandalizi ya uchaguzi wa leo lakini imesema vituo vyote 9,000 sasa viko tayari kutumiwa na wapiga kura watakaofika.
Kipindi cha kampeni za uchaguzi kiligubikwa na shutuma za wizi wa kura kwa upande wa chama tawala. Utafiti uliofanywa Zimbabwe na shirika moja lisilo la kiserikali mwezi Juni ulionyesha kwamba zaidi ya majina milioni moja yaliyosajiliwa katika madaftari ya wapiga kura yalikuwa ya watu waliokufa. Pamoja na hayo, zaidi ya watu laki moja wana umri wa zaidi ya miaka 100, jambo lililowafanya watafiti washuku uhalisia wa majina hayo.
Mugabe na Tsvangirai si wagombea pekee. Welshman Ncube ni mgombea wa urais wa chama cha MDCN kilichojitenga na chama cha MDC cha waziri mkuu Tsvangirai.
"Tunachotarajia ni uchaguzi wa haki. Tunachotarajia ni matokeo halali," alisema Nnube.
Tsvangirai apewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda
Zimbabwe bado inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Katika kampeni yake, Mugabe aliahidi kugawa mali ya nchi ili iweze kufikia wananchi maskini.
Kwa upande wake, Tsvangirai anataka kuwahimiza wawekezaji kutoka nje kufungua viwanda na biashara Zimbabwe. Ameahidi pia kutengeneza nafasi mpya za kazi milioni moja na kuboresha huduma kwa umma.
Maoni ya wapiga kura yanaonyesha kwamba Tsvangirai anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Asilimia 61 ya waliohojiwa walisema kwamba wanakipendelea chama cha MDC cha Tsvangirai huku asilimia 27 tu wakikiiunga mkono chama cha ZANU-PF cha Robert Mugabe.
Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa moja jioni kwa saa za Zimbabwe. Matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa katika kipindi cha siku tano zijazo.
Mwandishi:Elizabeth Shoo/afp/ap
Mhariri:Yusuf Saumu