1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamata kamata yaanza Zimbabwe

6 Juni 2013

Shirika la kutetea haki za binadamu ulimwenguni la Human Rights Watch limeitaka serikali ya mseto ya Zimbabwe kuhakikisha vyombo vya usalama vya nchi hiyo vinafanya kazi kwa misingi ya kazi yao na sio kumpendelea Mugabe.

https://p.dw.com/p/18lKh
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: Reuters

Katika ripoti yake ya kurasa 44, Human Rights Watch inalieleza jeshi la nchi hiyo na vyombo vingine vya ulinzi kuwa vimeingilia mambo ya kisiasa na uchaguzi kwa kumuunga mkono waziwazi Rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF, huku pia vikiwanyima raia wa Zimbabwe haki ya kutoa maoni na kupiga kura.

Ripoti hiyo imesema ushahidi wa hilo ni mwaka 2008 katika uchaguzi wa rais wakati jeshi la nchi hiyo lilipokiuka haki za binadamu kwa kufanya operesheni nchi nzima ya kupiga, kuadhibu na kuuwa wananchi.

Tokea kipindi hicho hadi leo, hakuna mabadiliko yaliyofanyika katika uongozi wa jeshi, vyombo vya usalama, polisi na shirika la ujasusi la nchi hiyo, na vyombo vyote hivyo vimebakia kama vilivyo hadi leo, vikimsaidia Rais Mugabe.

"Kutokana na vyombo vya usalama kuwa na haki ya kutishia na kuvamia wapinzani wa Mugabe, wananchi wa Zimbabwe hawana imani na uchaguzi mkuu huu wa nchi hiyo,'' Amesema Tiseke Kasambala mkurugenzi wa Human Rights Watch, ambaye ameongeza kwamba ili uchaguzi uwe na maana, serikali inatakiwa kuweke jeshi na vyombo vya usalama mbali na mambo yote ya uchaguzi.

Mageuzi ya vyombo vya usalama yanahitajika Zimbabwe

Tokea kuanzishwa kwa serikali ya muungano mwaka 2009, viongozi kadhaa wakuu wa jeshi la Zimbabwe wamekuwa wakimuunga mkono Rais Mugabe na chama chake cha ZANU-PF na kumfanyia ubaya Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na wenzake wa Vuguvugu la Mageuzi ya Kidemokrasia, MDC.

Polisi Zimbabwe
Polisi ZimbabwePicha: AP

Mei mosi mwaka huu kamishna mkuu wa jeshi la polisi nchini humo, Augustine Chihuri, alisema hadharani, vyombo vya usalama vya nchi hiyo haviwezi kufanya mazungumzo na Tsvangirai kuhusu kufanya mageuzi katika sekta ya ulinzi na kuwa yeyote atakayeripot hilo au kuzungumzia suala hilo anajiweka hatarini na atachukuliwa hatua.Tarehe 4 Mei 2013 kamanda wa jeshi la ulinzi la Zimbabwe, Jenerali Costantine Chiwenga, naye aliliambia taifa maneno hayo hayo ya kutofanya mazingumzo ya kufanya mageuzi katika vyombo vya usalama.

Shirika hilo limesema maelezo hayo ya upendeleo na vitisho ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini Zimbabwe, yamethibitishwa wazi katika vitendo vya vyombo vya usalama dhidi ya raia wa nchi hiyo.Tarehe 7 Mei mwaka huu, jeshi la polisi la nchi hiyo lilimtia mbaroni Dumisani Muleya mhariri wa gazeti huru la Zimbabwe na mwandishi wa gazeti hilo, Owen Gagare, baada ya gazeti hilo kuandika kuwa Tsvangirai amekutana na viongozi wa vyombo vya usalama.

Jeshi la polisi liliwaweka kizuizini watu hao wawili kwa muda wa saa nane na kuwashitaki chini ya sheria ya makosa ya jinai kwa kuchapisha maelezo waliyodai ni ya uongo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi hiyo.Uchunguzi uliofanywa na shirika hilo umegundua kuwa jeshi la la Zimbabwe limesambaza wanajeshi nchi nzima ili kutisha na kupiga wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa chama cha MDC na wakosoaji wa serikali ya Zimbabwe.

Kufuatia hali hiyo, shirika hilo limeitaka serikali ya Zimbabwe kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya viongozi wa vyombo vya usalama na kuhakikisha vyombo hivyo vinafuata maadili ya kazi zao ikiwemo kuwaadhibu viongozi wanaonekana kukiuka maadili hayo.

Mwandishi: Hasimu Gulana/Human Rights Watch

Mhariri: Mohammed Khelef