Zelensky aahidi ushindi dhidi ya Urusi
24 Februari 2024Zelensky amesema kwenye hafla ya kumbukumbu ya miaka miwili ya uvamizi kamili wa Urusi iliyofanyika mjini Kyiv kwamba wamekuwa wakipambana kwa siku 730 na watashinda.
Alikuwa akizungumza sanjari na Mawaziri Wakuu wa Canada, Italia na Ubelgiji pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, waliokwenda Kyiv kuonyesha mshikamano na Ukraine.
Von der Leyen amesema kupitia ukurasa wa X kwamba wanasimama na Ukraine kwa kila hali hivi sasa kuliko wakati wowote ule. Aidha alikabidhi magari 50 kwa jeshi la polisi la Ukraine na mamlaka zake za mahakama.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni anayekaimu uenyekiti wa kundi la mataifa tajiri ulimwenguni, G7 anatarajiwa kuongoza mkutano kwa njia ya mtandao kutokea Kyiv utakaohudhuriwa na Zelensky na viongozi wa Marekani, Italia, Canada, Uingereza, Japan, Ufaransa na Ujerumani.