1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Usalama wa chakulaAfghanistan

WFP kupunguza misaada ya chakula nchini Afghanistan

5 Septemba 2023

Shirika la Mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza Jumanne kuwa halitatoa msaada wa chakula mwezi huu kwa watu wengine milioni 2 wenye njaa nchini Afghanistan kutokana na upungufu mkubwa wa fedha.

https://p.dw.com/p/4Vz7N
Afghanistan | Erdbeben
Picha: Ahmad Sahel Arman/AFP/ Getty Images

Hatua hii mpya ya Mpango wa Chakula Duniani inamaanisha kuwa WFP itaweza kutoa msaada wa chakula kwa takriban theluthi moja ya watu milioni 15 ambao wanaihitaji chakula nchini Afghanistan.

Mkurugenzi wa WFP nchini Afghanistan Hsiao-Wei Lee amesema hali ya sasa nchini humo inatia wasiwasi na inagubikwa na njaa na utapiamlo, na kwamba kwa sasa katika utoaji wa misaada hulazimika kuwachagua wenye njaa zaidi huku mamilioni ya watu wakitaabika kupata chakula.

Lee amesisitiza kuwa kutokana na rasilimali chache walizonazo, hawawezi kuwahudumia watu wote ambao amesema wamo hatarini zaidi. Aidha Hsiao Lee amesema:

"WFP itawapunguza watu milioni 10 kwenye mpango wa msaada wa dharura wa chakula, kutoka milioni 13 hadi milioni 3. Na hivyo kutuacha tu na uwezo wa kusaidia mtu 1 kati ya 5 anayelala na njaa kila usiku. Hili haliwezekani na tulilishuhudia mwaka jana ambapo tuliweza kutoa msaada kwa watu milioni 23, jambo lililoepusha janga."

Soma pia: WFP- Upungufu wa misaada utazusha Baa la Njaa Afghanistan

Afghanistan, Kandahar | Ausgabe von World Food Programme Hilfsgütern
Raia wa Afghanistan wakipokea msaada wa chakula kutoka Shirika la WFP huko Kandahar 07.10.2021Picha: Sanaullah Seiam/Xinhua/picture alliance

Baadhi ya raia wa Afghanistan wametaja kushangazwa na hatua hiyo wakisema WFP inatakiwa kuongeza misaada ya chakula kuliko kuipunguza. Abdul Haq anaeishi katika makazi ya Woch Tangi anaeleza:

"Tulipokuwa tunapewa msaada, tuliishi maisha bora. Sasa, hatupati chochote. Tulikuwa tunakula milo mitatu kwa siku na baadaye milo miwili tu, na sasa tunakula mara moja tu kwa siku. Sio tu kwamba WFP inatakiwa kuendelea kutoa msaada, bali inapaswa kuuongeza. Kutokana na hali ngumu, kwa sasa vijana wamekuwa na fikra za kwenda nchi za kigeni kinyume cha sheria."

Uongozi wa Taliban wapelekea Afghanistan kutengwa

Taliban iliahidi kutawala kulingana na sheria zenye msimamo wa kati kuliko ilivyokuwa hapo awali wakati wa utawala wao katika miaka ya 1990. Lakini wamechukua hatua kali tangu kuchukua madaraka nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021 wakati vikosi vya Marekani na Jumuiya ya Kujihami NATO walipoondoka nchini humo baada ya miongo miwili ya vita.

Soma pia: UN: Afganistan inakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa

Miongoni mwa hatua hizo, Taliban wamepiga marufuku wanawake wa Afghanistan kufanya kazi katika mashirika ya ndani na yasiyo ya kiserikali. Mwezi Aprili, marufuku hiyo iliamriwa hadi kwa wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa.

Hatua hizo zilikosolewa vikali kimataifa, na kupelekea Afghanistan kutengwa zaidi wakati ambapo uchumi wake umedorora huku mgogoro wa kibinadamu ukizidi kuwa mbaya zaidi. Mashirika kadhaa yamekuwa yakitoa msaada wa chakula, elimu na afya kwa Waafghanistan baada ya Taliban kutwaa madaraka.

Kwa muda wa miezi sita ijayo, WFP inahitaji dola bilioni 1 ili kuwasaidia watu milioni 21 wanaohitaji msaada wa chakula ili kuokoa maisha yao.